December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Klabu za Fema zasherehekea miaka 20 tangu kuanzishwa

Spread the love

FEMINA Hip, kwa kushirikiana na Ubalozi wa Denmark na Sweden nchini Tanzania, wameadhimisha miaka 20 ya Klabu za Fema nchini Tanzania, jana, Novemba 16, 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Klabu za Fema ni jukwaa la aina yake lililoanzishwa na Femina Hip, ni Klabu za nje ya darasa ambazo zinafanya kazi katika shule za sekondari na vyuo vya kati kote nchini. Klabu za Fema ni mahali ambapo vijana hujitolea, hushirikishana na kujifunza stadi za maisha kupitia mafunzo mbalimbali.

Balozi wa Denmark hapa Tanzania, Mette Nørgaard Dissing‐Spandet alisema imekuwa nafasi ya heshima kubwa kufanya kazi na Femina Hip katika kubadilisha maisha ya vijana nchini Tanzania.

Alisema kupitia ushirikiano huo, wameona vijana wakianza kuishi mitindo bora ya maisha na kutoa mchango chanya kwenye ukuaji wa kiuchumi na kijamii.

“Vijana, nchini Tanzania na kote duniani, wanahitaji taarifa sahihi ili ziweze kuongoza maisha yao na nina furaha kushuhudia kwamba Femina Hip imetoa huduma hiyo kwa zaidi ya miongo miwili,” alisema Mwenyekiti wa Bodi Anna Mwasha.

Alisema katika siku zijazo, wanatarajia kufikia  shule za msingi, kwasababu ujuzi unaotolewa kupitia vyombo vya elimu ya Femina Hip (majarida ya kuchapisha, redio, mitandao ya kijamii, na majukwaa mengine ya kidigitali) ni muhimu kwa watoto wadogo pia.

Femina Hip imesajili zaidi ya klabu 2,370 katika shule za sekondari na vyuo vya kati, ikiwa na zaidi ya wanachama 230,000 kwa sasa.

Klabu hizi zinapewa msaada na walimu washauri zaidi ya 2,720 wanaojitoa na kujitolea, ambao ni walimu katika shule husika, pamoja na mtandao wa waliowahi kuwa wanachama wa Klabu za Fema. Walimu washauri wa klabu hawafanyi kazi peke yao; wameungana kuunda mitandao 81 Tanzania nzima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Femina Hip, Ruth Mlay alisema wanayo furaha kutangaza kwamba ni miaka miaka 20 sasa tangu klabu ya kwanza ilipoanzishwa Liwale, Lindi.

Alisema katika kipindi cha miaka 20 iliyopita, Klabu za Fema zimewashirikisha moja kwa moja na kuwainua zaidi ya vijana milioni 15 ambao nao wamebeba maadili, mitazamo, na ujuzi waliojifunza katika klabu na wakaingia nao katika taaluma zao, familia, na maisha ya kijamii.

Femina Hip ni asasi kubwa zaidi ya kiraia inayolenga vijana nchini Tanzania iliyojikita katika kuhamasisha, kusaidia na kuelimisha vijana wenye umri wa miaka 10 hadi 30.

Shirika hili huchapisha majarida, kuzalisha vipindi vya redio na televisheni, kampeni za mitandao ya kijamii na bidhaa nyingine za kidigitali ili kukuza mitindo bora ya maisha, afya ya uzazi, ushiriki wa kiraia, uwezeshaji kiuchumi na usawa wa kijinsia. Kwa miaka mingi Femina Hip imefadhiliwa na serikali za Denmark na Sweden ili kutekeleza shughuli zake.

error: Content is protected !!