December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kizimbani kwa utakatishaji Bil. 1.5, asomewa mashtaka 106

Spread the love

 

GASTON Danda, mfanyabiashara na mkazi wa Mbezi Beach, Kinondoni jijini Dar es Salaam, amepandishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Kwa makosa ya kughushi nyaraka na utakatishaji fedha kiasi cha Sh. 1.5 bilioni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Danda amesomewa mashtaka hayo leo Jumanne, tarehe 8 Novemba 2022, na Wakiki wa Serikali, Yusph Aboud, akisaidiana na Wakili wa Serikali, Adolf Verandumi, mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Pamela Mazengo.

Mawakili hao wa Serikali wamemsomea Danda mashtaka 106, anayodaiwa kufanya kati ya tarehe 26 Agosti hadi 10 Novemba, 2020, maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam.

Miongoni mwa mashtaka hayo ni utakatishaji wa Sh. 1,569,600,000 (Bil. 1.5), kinyume cha kifungu Cha 12(d) na 13(a) cha Sheria ya Utakatishaji Fedha.

Shtaka lingine ni la kughushi nyaraka iliyotambulishwa Kwa barua ya tarehe 26 Oktoba 2020, Kwa lengo la kuonyesha Johnson Masalu Clement ni Mwajiriwa wa Kampuni ya Savana Mining Limited, huku akijua ni kosa kisheria.

Anadaiwa kulitenda tarege 26 Oktoba 2020, jijini Dar es Salaam, kinyume cha kifungu cha 333, 335 (a) na 337 cha Sheria ya Kanuni za Adhabu.

Shtaka lingine ni la kujipatia fedha kinyume cha kifungu Cha 302 Cha Sheria ya Kanuni za Adhabu, ambapo anadaiwa tarehe 31 Oktoba 2020, katika Benki ya CRDB, tawi la Msasani, Kwa lengo la udanganyifu alijipatia Sh. 49 milioni kupitia akaunti No. 152530187600, yenye jina la Johnson Masalu Clement.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Mazengo alimueleza mshtakiwa huyo anayewakilishwa na Wakili Edward Hoseah, kwamba hawezi kujibu kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za utakatishaji fedha.

Hakimu Mazengo amesema kuwa, kesi yake itahamishiwa katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar es Salaam, pindi upelelezi wake utakapokamilika.

Baada ya Hakimu Mazengo kutoa maelezo hayo, Wakili Aboud aliomba kesi hiyo iahirishwe Kwa kuwa upelelezi wake haujakamilika.

Hakimu Mazengo aliahirisha kesi hiyo hadi tarehe 22 Novemba 2022, ambapo itasikilizwa Kwa njia ya video. Amesema mtuhumiwa ataendelea kubaki rumande Kwa kuwa mashtaka yanayomkabili haina dhamana.

error: Content is protected !!