SUSAN Kiwanga na wenzake wawili, wameshindwa kurithi nafasi ya Halima Mdee ya Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha). Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).
Mbali na Kiwanga, wengine ni Monica Nsaro wa Tabora na Aisha Luja wa Singida ambao walijitosa kuchukua fomu za kuwania kukaimu nafasi hiyo iliyoachwa na Mdee.
Kiwanga ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, aliyewahi kuwa mbunge wa Mlimba, Mkoa wa Morogoro kwa pamoja, wameshindwa kushika wadhifa huo kwa mujibu wa Katiba ya Chadema.
Badala yake, Kamati tendaji ya Bawacha, inakutana kesho Jumanne tarehe 18 Mei 2021, jijini Mwanza kwa ajili ya kujaza nafasi za katibu mkuu, naibu katibu mkuu Bara, naibu katibu mkuu Zanzibar, katibu mwenezi na makamu mwenyekiti wa Bawacha-Bara.
https://www.youtube.com/watch?v=sz54_1uWwIY
Nafasi hizo, zinajazwa baada ya kamati kuu ya Chadema, tarehe 27 Novemba 2020, kufukuzwa uanachama, kwa tuhuma za usaliti, kughushi nyaraka za chama kisha kujipeleka bungeni Dodoma kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum.
Nafasi zingine ambazo zinajatwa ni; katibu mkuu, naibu katibu mkuu bara na Zanzibar na mratibu wa uenezi.

Nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti Bara ambazo wanachama wa Chadema walijitosa kuchukua fomu, zimewekwa kando kutokana na Katiba ya Chadema, kutokuonyesha, ikiwa nafasi ya mwenyekiti itakuwa wazi, kutafanyika uchaguzi wa kuijaza.
Hoja hii imepata mashiko na kilichotokea kwa Baraza la Vijana la Chadema, (Bavicha), wakati aliyekuwa mwenyekiti wake, Patrobas Katambi alipotimkia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Novemba 2017, Patrick Ole Sosopi, aliyekuwa makamu mwenyekiti-Bara wa baraza hilo, alithibitishwa na kamati tendaji kuwa mwenyekiti.
Kwa msingi huo, Sharifa Suleiman ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Bawacha-Zanzibar, ndiye amechukua nafasi ya Mdee ya Mwenyekiti wa Bawacha.
Nafasi ya makamu mwenyekiti wa Bawacha-Bara na Zanzibar, watateuliwa miongoni mwa wajumbe wa kamati tendaji inayoundwa na wenyeviti na makatibu wa mikoa pamoja na wajumbe wa kamati kuu ambao ni wanawake.

Ndiyo maana, taarifa iliyotolewa juzi Jumamamosi na Singo Kigaila Benson, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Bara, kuhusu kujazwa kwa nafasi hiyo za Bawacha, hakuna wagombea wa nafasi ya mwenyekiti na makamu mwenyekiti.
Kigaila alisema, kamati kuu ya chama hicho, iliyokutana kwa njia ya mtandao, ilijadili na kuteua wagombea ambapo nafasi ya katibu mkuu walioteuliwa ni; Asia Msangi, Catherine Rugen a Esther Daffi.
Naibu katibu mkuu Bara wako watatu; Brenda Jonas, Emma Boki na Nuru Ndosi huku upande wa Zanzibar kwa nafasi hiyo akiwa mmoja, Bahati Haji.
Mratibu mwenezi wa Bawacha wako watatu ambao ni; Aisha Ame, Husna Said na Singrada Mligo.
Mbali na Mdee aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), wengine ni, waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko, pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.
Katika orodha hiyo, wamo pia Hawa Subira Mwaifunga, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa katibu mwenezi na Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar na Katibu Mkuu, Bawacha-Bara, Jesca Kishoa.
Pia, aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.
Wengine waliofukuzwa Chadema, Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.
Leave a comment