April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kiwanga ajitosa kuwania ‘kiti cha Mdee’

Spread the love

 

JINA la Susan Kiwanga, limeingia kwenye orodha ya wanachama wa Chadema wanawania nafasi ya Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha) Taifa. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Kiwanga ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, amerejesha fomu ya kuomba nafasi hiyo leo Jumatatu tarehe 15 Machi 2021, makao makuu ya chama hicho Kinondoni, mkoani Dar es Salaam.

Nafasi hiyo inagombewa baada ya aliyekuwa mwenyekiti wake, Halima Mdee kuvuliwa wadhifa huo sambamba na kuvuliwa uanachama wa chama hicho kwa kosa la usaliti, tarehe 27 Novemba 2020.

 

Akizungumza baada ya kurejesha fomu hiyo, Kiwanga, aliyewahi kuwa mbunge wa viti maalum 2010-2015 na mbunge wa Mlimba mkoani Morogoro 2015-2020 amesema, amejitosa katika kinyang’anyiro hicho, ili kuziba pengo lililoachwa na Mdee.

Mbali na hilo, Kiwanga amesema, amemua kugombea baada ya kuona kuna ombwe kubwa la uongozi ndani ya Bawacha.

“Kuna mambo mengi yamepita lakini hakuna matamko yanayotolewa, kuna ombwe la uongozi kwenye baraza. Kuna mambo hayajanifurahisha, nikaona nijitose kugombea nafasi hii,” amesema Kiwanga

“Mfano hili tatizo la COVID-19 walitakiwa kutoa tamko, sababu wanaoathirika ni kina mama na watoto lakini tumekaa kimya kwa muda mrefu. Kina mama ilitakiwa tuseme lakini utawezaje kama sio kiongozi?” amehoji Kiwanga.

Amesema, akifanikiwa kuipata nafasi hiyo, atatekeleza wajibu wake bila woga “Sio mimi tu, wanawake wa Chadema tuko vizuri na hasa akipata mtu yeyote. Sisi wanawake Chadema tukikusanyika hata 10 tunakuwa tuko kama 1,000.”

“Na kama mtu ataogopa, tutamwambia kaa pembeni sisi hatuogopi kama jela, rumande tumekaa sana,” amesema Kiwanga.

Bawacha linatarajia kufanya uchaguzi kujaza nafasi zilizoachwa wazi baada ya Mdee na wenzake kufukuzwa Chadema.

Nafasi hizo ni pamoja na Katibu Mkuu, Makamu Mwenyekiti Bara, Naibu Katibu Mkuu na Katibu Mwenezi.

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa Chadema 27 Novemba 2020, kwa tuhuma za usaliti kutokana na kujipeleka bungeni kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu bila idhini ya chama chao.

Wengine waliofukuzwa ni, waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu Chadema Ester Bulaya na Esther Matiko; aliyekuwa Katibu wa Baraza la Vijana Chadema (Bavicha), Nusrat Hanje na Grace Tendega, aliyekuwa Katibu Mkuu Bawacha.

Hawa Mwaifunga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti Bawacha Bara; Jesca Kishoa, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Bawacha na aliyekuwa Katibu Mwenezi Bawacha, Agnesta Lambart.

Poa wamo Tunza Malapo, Cecilia Pareso, Asia Mwadin Mohamed, Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Siyao, Salome Makamba, Anatropia Theonest na Conchestea Lwamlaza.

Mwanasiasa huyo na wenzake, waliapishwa na Job Ndugai, Spika wa Bunge tarehe 24 Novemba 2020, kuwa wabunge wa viti maalumu wakati Chadema.

Chadema kiliweka msimamo wa kutopeleka wawakilishi wake bungeni, kikipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu wa 2020 kwamba uligubikwa na hila.

Mbali na nafasi hiyo inayowania ya kaimu mwenyekiti, nyingine ni; kaimu makamu mwenyekiti-Bara, katibu mkuu, naibu katibu mkuu bara na Zanzibar pamoja na katibu mwenezi wa baraza hilo.

error: Content is protected !!