August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kiwanda chamuumbua Waziri Mwijage

Spread the love

SERIKALI imeendelea kupata kigugumizi juu ya ufufuaji wa kiwanda cha General tyre, kilichopo mkoani Arusha licha ya kutoa ahadi ya kukifufua kiwanda hicho mwezi Juni mwaka 2016 katika Bajeti ya iliyopita ya serikali, anaandika Dany Tibason.

Serikali ilitenga Sh. 150 milioni kwa ajili ya kusaidia ufufuaji wa kiwanda hicho, lakini mpaka sasa Charles Mwijage, Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko ameshindwa kueleza hatima ya kiwanda hicho.

Akizungumza bungeni leo wakati akijibu swali la Saed Kubenea, Mbunge wa Ubungo kuhusu hatima ya kiwanda hicho amesema serikali imeshindwa kurejesha shughuli za kiwanda hicho kwani utafiti umebaini kuwa mitambo yake ni kongwe isiyofaa kuzalisha bidhaa za ushindani.

“Kwa sasa, Serikali inamiliki kiwanda cha General tyre kwa asilimia 100 na tumefanya utafiti kuhusu uwezo wa teknolojia itakayotumika kuendesha kiwanda hicho pamoja na upatikanaji wa malighafi.
“Taarifa za awali zimebaini kuwa mitambo iliyopo ambayo ilifungwa kwenye miaka ya 60 na haifai kwa uzalishaji wa kiushindani,” amesema.

Awali katika swali lake, Kubenea alitaka kujua ni lini serikali itakamilisha ufufuaji wa kiwanda hicho kama ambavyo imekuwa ikitoa ahadi mara kwa mara?

Waziri Mwijage amekiri kuwa ufufuaji wa kiwanda hicho bado ni kitendawili na kwamba dhamana ya kusimamia kiwanda hicho kwa sasa ipo chini ya Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC), na dhamira ya Serikali ni kuona kiwanda kiwanda hicho kinaanza kuzalisha matairi mapema ingawa hakueleza ni lini kitaanza.

error: Content is protected !!