February 28, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kiwanda cha nguo chapongezwa kuzuia uchafuzi wa mazingira

Spread the love

KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Charles Francis kabeho amezingdua mradi wa kuchakata maji taka kwenye kiwanda cha nguo 21st Century wenye thamani ya Sh. 1.8 bilioni huku akiupongeza uongozi wa kiwanda kwa kusaidia kuzuia uchafuzi wa mazingira katika eneo la viwanda. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Kabeho amesema kuwa mradi huo umeonesha manufaa mengi baada ya kuendelea kuongeza ajira kufuatia mabaki ya taka kutumika kutengeneza matofali ambayo yanasaidia kiwandani humo, huku kikiendela kutoa kodi kwa Serikali.

Awali Ofisa uhusiano wa kiwanda hicho, Steven Mlambiti amesema kuwa mradi huo ulianza kujengwa kwa awamu ya kwanza tangu mwaka 2016 ambapo ulikamilika mwaka 2017 na kuwekwa jiwe na msingi na mkimbiza mwenge wa Uhuru.

Amesema kuwa awamu ya pili ya ujenzi ilihusisha bwawa na mapokezi ya maji baada ya kuchujwa lenye ujazo wa lita 500,000 sambamba na ujenzi wa bwawa la kupokea maji yaliyosafishwa na kurudishwa tena kiwandani kwa matumizi ya uzalishaji lenye ujazo wa lita 300,000.

Hivyo Mlambiti amesema kuwa kufuatia ujenzi wa mitambi hiyo uliofanywa na kampuni ya Lon Exchange India ya nchini India, uchakataji huo umefanikisha kutiririshaji wa maji yasiyo safi na madhara katika mito kupungua kwa asilimia 60.

Mlambiti amesema, mradi huo umewezesha kuwepo kwa hifadhi ya mazingira kwa kuondoa kero ya utiririshaji wa maji yenye sumu kwenye makazi ya wananchi.

Pia alitaja manufaa mengine ya mradi kuwa ni umewezesha pia upatikanaji wa maji ya kutosha kwa matumizi ya kiwanda kuendeshea mitambo na kupunguza gharama za matumizi ya maji kwa 30% na kuondoa kero ya mgao wa maji unaofanywa na mamlaka ya maji safi na maji taka MORUWASA ambayo huathiri uzalishaji kiwandani kufuatia kiwanda kuwa kilikuwa kikitumia karibu lita bil 3 kwa siku ambapo kwa sasa kinatumia lita bililioni moja pekee za kutoka MORUWASA.

Aidha amesema kiwanda kimeweza kutoa ajira kwa vijana wazawa wapatao 3000 ambapo miongoni mwao wakiwa wanawake ni asilimia 45 na wanaume ni asilimia 55 pamoja na raia wa kigeni 50.

Awali Mkuu wa wilaya ya Morogoro, Regina Chonjo amesema kuwa kiwanda hicho ni kiwanda cha muda mrefu huku kikiwa ni moja ya viwanda vilivyobinafsishwa lakini kinaendelea na uzalishaji wa vitenge kwa kutumia pamba kwa kuichakata kuanzia shambani hadi vitenge huku kikiwa ni kiwanda pekee Tanzania kinachozalisha nguo za majeshi mbalimbali.

Mwenge wa Uhuru upo mkoani Morogoro ukitokea Mkoa wa Pwani ambapo kwa sasa upo wilayani Morogoro vijijini ukiendelea kuzindua miradi ya maendeleo ili kukamilisha miradi 57 yenye thamani ya zaidi ya shilingi Bilion 18 iliyokusudiwa kuzinduliwa.

error: Content is protected !!