August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kiwanda cha mafuta matatani, wafanyakazi walia

Spread the love

UONGOZI wa kiwanda cha mafuta cha Tanzania Murzah Oil Mill unalalamikiwa kugoma kulipa mafao ya waliokuwa wafanyakazi wa kiwanda hicho baada ya kubinafsishwa kwake, jambo linalozidi kuchochea mgogoro baina ya pande hizo mbili, anaandika Aisha Amran.

Aidha wafanyakazi wa kiwanda hicho, wamelalamikia kuwa, uongozi wa kiwanda hicho pia umekataa kutoa ushirikiano kwa Shirikisho la Wafanyakazi wa Taasisi za Fedha na Viwanda Tanzania (TUICO) ilipojaribu kutatua mgogoro huo baina ya mwajiri na wafanyakazi.

Wafanyakazi wa kiwanda hicho walifikisha malalamiko yao kwa mwajiri baada ya kiwanda kubinafsishwa ili walipwe mafao yao, ikiwemo kulipwa 10% kama Sheria ya Ajira na Mahusiano ya Kazi ya mwaka 2014 inavyoeleza. Hata hivyo juhudi zao zimegonga mwamba.

Mwajiri wa kiwanda hicho, anadaiwa kushindwa kuwalipa kiasi hicho cha fedha na badala yake kuwalipa 5% kama sehemu ya mafao yao jambo ambalo ni kinyume na sheria.

Rashid Kiswago, Mwenyekiti wa wafanyakazi hao amesema, mwajiri ameamua kulipa kiasi hicho ambacho si makubaliano yao wala matakwa ya sheria na pia fedha hizo hazina mchanganuo.

Wafanyakazi wengine, ambao hata hivyo hawakuwa tayari kutajwa majina yao wamesema, kuna mchezo mchafu unachezwa kati ya uongozi wa kiwanda hicho na Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi kavu (SUMATRA) jambo linalosababisha kupotea kwa haki zao.

“Mikataba yetu ya kazi ipo SUMATRA kwa upande wa madereva lakini hatujawahi kusaini mikataba hiyo tangu tuanze kazi zaidi ya miaka kumi sasa,” amesema mmoja wa wafanyakazi hao na kuongeza;

Mikataba ya madereva iliyopo SUMATRA inaonyesha tunalipwa laki sita (600,000), lakini hapa kwenye kampuni hakuna mikataba na tunalipwaa shilingi laki mbili (200,000) kwa mwezi.

Mwanahalisi Online imeutafuta uongozi wa kiwanda hicho ili kujibu madai ya wafanyakazi hao pasipo mafanikio, hata hivyo, mmoja kati ya watu anayedaiwa kuwa kiongozi wa kampuni ambaye hakutaka kujitambulisha jina kwa madai kuwa yeye siyo msemaji wa kiwanda hicho amesema;

“Hatujamfukuza kazi mtu yoyote hivyo, hatuwezi kuwalipa kiasi hicho cha mafao wanachokidai kwa mujibu wa sheria bali tutawahamishia kwa mmiliki mpya wa kiwanda na wataendelea na ajira zao.”

error: Content is protected !!