Friday , 19 April 2024
Home Gazeti Tangulizi Kivuko chakwamisha wananchi Mafia zaidi ya siku tatu
Tangulizi

Kivuko chakwamisha wananchi Mafia zaidi ya siku tatu

MV Kilindoni
Spread the love

 

WANANCHI wilayani Mafia wameilalamikia kukosekana kwa huduma ya usafiri wa kuvuka kuingia na kutoka kisiwani humo kwa zaidi ya  siku tatu huku wakiomba Serikali ifungue milango kwa wawekezaji binafsi kufanya kazi hiyo. Anaripoti Faki Sosi, Pwani … (endelea).

Mwandishi wa Habari hizi alipigiwa simu na wananchi waliokwama kwenye bandari ya Nyamisati kwa siku tatu tangu tarehe 29 Septemba hadi tarehe Mosi Oktoba mwaka huu huku siku zinazofuata wakisafiri kwa msaada wa meli ya kijeshi MV Songosongo ambayo pia hakikuweza kutoa huduma hiyo siku zote na kupelekea wananchi kuendelea kushindwa kusafiri kwa wakati.

Mwandishi wa Habari hizi alifika kwenye bandari ya Nyamisati ambapo alizungumza na baadhi ya wananchi waliokuwa wakisubiri usafiri bandani hapo.

Nassir Ali mkazi wa Kiegeni Mafia aliyekwama bandari hapo tangu tarehe 29 alisema kuwa kuna kila sababu ya serikali kuachana na biashara ya usafirishaji wa wananchi kwa sababu wameonyesha kushindwa tangu wanaanza.

“Mafia sio mbali pa kusafiri kwa saa tano hapa serikali iwafungulie milango wawekezaji walete boti  isafirishe watu kwa boti nzuri ya kisasa hapa tunavuka kwa saa moja,” amesema.

Nassir amesisitiza Serikali iwatafute wawekezaji kwa kuwa uchumi wa kisiwa cha Mafia unategemea usafiri wa bahari  “hakuna mwekezaji atakayekataa kwani kutoka mafia kwenda Nyamisati kuna idadi ya watu 300 kila siku ni uwekezaji wenye tija hakuna mfanyabiashara atakayekataa wawaombe kina Mzee Bakharesa.”

Hamima Rashid alisema kuwa yeye na watoto wake wawili mmoja ana miaka miwili na mwengine ana miaka 11 wapo hapo kwa siku mbili na kwamba wapo aliowakuta hapo walioshindwa kusafiri kwa sababu ya kukosekana kwa kivuko.

“Tumeambiwa Kivuko kibovu na hatujui lini kitapona ndio tupo hapa tunasubiri hatma yetu,” amesema Hamima.

Alafi Juma amesema kuwa watu wamelazimika kusafiri kwa boti za kienyeji  ili wawahi kwenye mipango jambo ambalo ni hatari.

“Watu wanaweka reheni roho zao ni lini hasa mafia tutakuwa na uhakika wa usafiri kama wenzetui wa unguja kwa sisi sio wananchi wananchi wa nchi hii tunaomba kilio chetu kimfikie Rais Samia atusaidie,” amesema Juma.

Amani Omar Mkazi wa Kilindoni Mafia amesema “ifike pahala shida ya usafiri iishe ili wananchi wazungumzie maendeleo  hakuna maendeleo ya Mafia bila kuimarisha usafiri wa bahari kwa kuwa kisiwa hiKI kinategemea bidhaa nyingi kutoka Dar es Salaam na sehemu nyengine bara.”

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Martin Ntemo, akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi kwa njia ya simu ameelekeza shukrani zake kwa Jeshi la Wananchi (JWTZ) kwa kutoa meli yao MV Songosongo kwa ajili ya kuwasaida wananchi  kupata nafuu ya usafiri kwa wakati huu wa dharura.

DC Ntemo amekiri kuwepo kwa shida ya usafiri ambapo alieleza kuwa tayari Serikali ya Halmashauri ishachukua hatua za haraka kwa kuwasiliana na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makeme Mbarawa na kuwasilisha ombi la kutaka Halmashauri kuendesha  Kivuko hicho ambacho kipo chini ya Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa).

“Kwa kweli wenzetu wa Temesa wanatuangusha huduma zao ni duni hivyo tumewasilisha ombi kwa Waziri wa Ujenzi kwamba sisi Halmashauri tukisimamie chombo hiki cha Jeshi ili kuokoa wananchi  wetu,” amesema DC Ntemo.

Amesema kuwa licha ya wananchi kukosa usafiri lakini tatizo hilo linapelekea kukwama kwa miradi ya serikali  kwa sababu hivyo Vivuko ndivyo vinavyobeba mizigo ya kuwezesha miradi hiyo.

Amesema kuwa hali hiyo inapelekea wananchi kusafiri kwenye vyombo visivyo salama bahari “wananchi wakikosa Kivuko wanatumia hivi vyombo hatarishi na wengi husafiri na watoto wadogo  na wagonjwa”.

Mwaka 2020 kampuni binafsi ya MV Capten 1 ilipewa tenda ya kusafirisha abiria kutoka Mafia kwenda bandari ya Nyamisati na baadaye Mwaka 2021 Serikali ilipeleka Kivuko cha MV Kilindoni ikapelekea kupunguza tatizo la usafiri kisiwani humo ambapo kwa sasa vyombo hivyo ni vibovu na kupelekea shida ya usafiri kisiwani humo.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari za SiasaTangulizi

Tanzania, Uturuki zanuia kukuza biashara, uwekezaji

Spread the loveSERIKALI za Tanzania na Uturuki zimekubaliana kuendeleza dhamira ya kuimarisha...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

Habari za SiasaTangulizi

Rais Samia kutunukiwa udaktari wa heshima Uturuki

Spread the loveBaraza la Chuo Kikuu cha Ankara, ambacho ni cha pili...

error: Content is protected !!