August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kitwanga: Sijutii kutumbuliwa

Spread the love

CHARLES Kitwanga, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi amesema kuwa, hajutii ‘kutumbuliwa’ na Rais John Magufuli, anaandika Moses Mseti.

Ametoa kauli hiyo wikiendi iliyopita jimboni kwake Misungwi jijini Mwanza ikiwa ni takribani mwezi mmoja baada ya kung’olewa kwenye nafasi hiyo.

Kitwanga alifukuzwa kazi kwa madai ya kuingia bungeni na kujibu masali ya wizara yake akiwa amelewa.

Amesema kuwa, anamshukuru Mungu kwa kuondolewa katika nafasi hiyo na kwamba, huenda kama angeendelea kuwepo, angepata matatizo makubwa zaidi.

Na kwamba, hatua ya Rais Magufuli kumwondoa katika nafasi hiyo kitamsaidia kuwatumikia wananchi wa jimbo lake kwa ukaribu zaidi tofauti na alivyokuwa kwenye nafasi ya uwaziri.

“Namshukuru sana Mungu kuondolewa katika nafasi hii (Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi) labda ameniepusha na mambo mengi ambayo yangeweza kunikumba na hii itanisaidia kuwatumikia wanamisungwi kwa ukaribu,” amesema Kitwanga.

Kitwanga baada ya kung’olewa katika nafasi hiyo, siku kadhaa baadaye alitimkia nchini Israel ambako inadaiwa kwenda kupumzika ambapo alirejea nchini hivi karibuni.

Baada ya kurejea nchini, Kitwanga moja kwa moja alikabidhiana Ofisi na Waziri wa Mambo ya Ndani kwa Mwigulu Nchemba aliyeteuliwa kushika nafasi hiyo. Nchemba alikuwa Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi.

Kabla ya kutimuliwa Kitwanga alikuwa akiandamwa na kashfa ya Kampuni ya Lugumi iliyopewa zabuni ya kufunga mashine za kutambua alama za vidole katika vituo vyote vya Jeshi la Polisi nchini.

Jeshi hilo liliingia mkataba na Kampuni ya Lugumi Enterprises ili kufunga mashine 108 nchi nzima lakini kampuni hiyo ilifunga mashine 14 tu.

error: Content is protected !!