August 8, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kitwanga lawamani Misungwi

Charles Kitwanga, Mbunge wa Jimbo la Misungwi

Spread the love

NICODEMUS Ihano, diwani wa kata ya Mabuki wilayani Misungwi amemtupia lawama Charles Kitwanga, Mbunge wa Jimbo la Misungwi akidai ni miongoni mwa ‘vigogo’ wanaowalinda wakandarasi wazembe katika halmashauri ya wilaya hiyo, anaandika mwandishi wetu.

Mwingine anayelaumiwa kwa kuwalinda wakandarasi wanaofanya kazi chini ya kiwango katika miradi mbalimbali ni Antony Bahebe, mwenyekiti wa halmashauri ya Misungwi.

Ihano ameyasema hayo wakati akichangia hoja katika kikao cha baraza la Madiwani kilichofanyika wilayani hapa ambapo aliwashutumu wakandarasi kwa kufanya kazi chini ya kiwango huku wakikilindwa na viongozi wa juu wa halmashauri hiyo.

“Antony Bahebe, mwenyekiti wa halmashauri yetu anafanya jitihada za kuzuia uwazi katika kujadili hoja zenye maslahi kwa wananchi kwa madai ya kuenda na muda, kitendo ambacho ni njama za kuficha ukweli,” alisema na kuongeza;

“Tumeshangazwa na jinsi mwenyekiti wetu alivyozuia hoja zisijadiliwe kwa kina ili kuficha ukweli. Ifike mahala tuachwe tujadili uozo uliopo katika halmashauri yetu kwa maslahi ya
wananchi wetu.”

Ihano amesema “Hatujui kuna ajenda gani iliyo nyuma ya pazia kwani hata Kitwanga ambaye ni mbunge wetu amekuwa akiwatetea sana wakandarasi wanaofanya kazi kwa mazoea na kuchelewesha ukamilishaji wa miradi ya maedeleo.”

Awali kabla ya kuanza kwa kikao hicho, Juma Sweda ambaye ni Mkuu wa Wilaya ya Misungwi alipokaribishwa kutoa salamu za serikali aliweka bayana uozo aliojionea wakati alipofanya ziara yake katika wilaya na kusema kuwa baadhi ya madiwani ni wakwepa kodi wakubwa.

“Naomba niwe mkweli jamani, miongoni mwa wanaokwamisha maendeleo ya Misungwi katika ukusanyaji wa mapato ni pamoja na wafanyabiashara wakubwa mkiwemo ninyi madiwani.

Kuanzia sasa tutaanza kuwafuatilia mlipe kodi zote kuanzia ile ya miaka ya nyuma hadi sasa na msipofanya hivyo tutawachukulia hatua kali,” alisema Sweda.

error: Content is protected !!