September 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kitilya, Sinare kizimbani kwa kuibia serikali

Spread the love

HARRY Kitillya, aliyekuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA); Shose Sinare, Mkuu wa Idara ya Ushirikiano na Uwezekezaji katika Benki ya Stanbic na Sioi Solomoni, mwanasheria wa benki hiyo, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa kosa la kughushi nyaraka za serikali ili kujipatia pesa, anaaandika Faki Sosi.

Akiwasomea mashtaka, Stanley Luoga, Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), mbele ya Amili Mchaura, Hakimu Mkazi Kisutu, amesema vigogo hao walighushi nyaraka hizo kati Agosti 2012 na Machi 2013 jijini Dar es Salaam.

Luoga ameieleza mahakama kuwa kosa la pili limefanywa na Sinare tarehe 2 Agosti mwaka 2012, kwamba alighushi hati ya mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni katika Benki ya Stanbic ya Tanzania na Benki ya Standard ya Uingereza akiiombea fedha Serikali ya Tanzania.

Sinare anatuhumiwa kwa kosa la tatu alilotenda tarehe 13 Agosti 2012, la kupeleka hati ya kughushi kwenye Wizara ya Fedha iliyoonesha kuwa Serikali ya Tanzania itapewa mkopo wa Dola za Marekani 550 milioni kutoka Benki ya Stanbic ya Tanzania na Standard ya Uingereza.

Washitakiwa wote wanakabiliwa na kosa la kutengeneza mkataba bandia tarehe 5 Novemba mwaka 2012 Jijini Dar es Salaam kwenye Makao Makuu ya Benki ya Stanbic kupitia Kampuni ya Enterprise Growth Market Advisor (EGM).

Shitaka jingine linalowakabili watuhumiwa wote ni usafirishaji haramu wa fedha kati ya mwezi Machi 2013 na Septemba 2015.

Kiasi cha Dola za Marekani milioni sita zilihamishwa kutoka kwenye akaunti namba 0240026633702, 0240026633701 na 9120001251935 za Kampuni ya EGMA kwenye Benki ya Stanbic na kupelekwa kwenye akaunti namba 3300605539 na 3300603692. Akaunti hizo zinamilikiwa na kampuni ya EGMA.

Washitakiwa wote wamekana mashitaka yote na wamenyimwa dhamana. Uamuzi wa dhamana yao utatolewa tarehe 8 Aprili mwaka huu.

error: Content is protected !!