October 2, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Kitanzi’ cha AZAKI chalalamikiwa

Spread the love

ASASI za Kiraia nchini (AZAKI) pamoja na watetezi wa haki za binadamu, wameiomba serikali kuondoa bungeni muswada wa mabadiliko ya Sheria ya Kampuni na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali (NGO’S), uliouwasilisha bungeni kwa hati ya dharura hivi karibuni. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Ombi hilo limetolewa tarehe 24 Juni 2019 na wadau wa AZAKI katika mkutano wao wa dharura uliolenga kujadili muswada wa mabadiliko ya sheria mbalimbali zinazo ongoza asasi za kiraia, Jijini Dar es Salaam.

Wadau hao wameeleza kuwa, baadhi ya vifungu katika muswada huo vinakwenda kinyume na katiba pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, kutokana na kuminya uhuru wa AZAKI nchini.

Onesmo Olengurumwa, Mratibu wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) ameeleza kuwa, baadhi ya vifungu vya muswada huo vinampa mamlaka makubwa Msajili wa NGO’S katika kusimamia mashirika hayo ikiwemo kuwa na mamlaka ya kufuta usajili wake bila kufuata taratibu za kisheria.

Pia, Olengurumwa amesema baadhi ya vifungu vya muswada huo vinaminya uhuru wa AZAKI katika kutekeleza majukumu yake ikiwemo kutetea haki za binadamu kutokana kwamba vifungu hivyo havitambui masuala ya utetezi wa haki za binadamu.

“Miongoni mwa changamoto hizo ni kuminywa uhuru wa AZAKI nchini kinyume na katiba pamoja mikataba ya kimataifa ambayo Tanzania imeridhia, msajili wa NGO’s amepewa mamlaka makubwa ya namna ya kusimamaia asasi za kiraia ikiwa pamoja kufuta usajili wa AZAKI bila kufuata utaratibu wa kisheria, “ amesema Olengurumwa na kuongeza.

“Muswada huu utazitaka asasi zote zilizosajiliwa chini ya sheria ya makampuni ambayo hayakuomba hati ya kukubaliwa kufanya kazi kama mashirika yasiyo ya kiserikali, yatatakiwa kufanya kazi kama makampuni ya kibiashara na iwapo yatashindwa kufanya hivyo ndani ya muda wa miezi miwili watafutiwa usajili.”

Zitto Kabwe, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo amesema, iwapo miswada hiyo itapitishwa na kuwa sheria, mashirika mengi yanayojishughulisha na uwezeshaji jamii, ikiwemo zizotoa misaada katika sekta ya afya, elimu na uwezeshaji, yatafungwa na kunyima wananchi huduma hizo.

“Sheria ya NGO’s tunajua lengo lake ni nini, kama mnavyofahamu mashirika makubwa ya kutetea haki za binadamu,  masuala ya uwajibikaji kama vile LHRC,TGNP ,TWAWEZA , yamesajiliwa kwa kupitia sheria ya makampuni kifungu kinachohusiana na makampuni yasiyotengeneza faida,

“Na hii ilikuwa inawapa uhuru sababu kwa mujibu wa sheria msajili wa makampuni hana mamlaka ya kufuta kampuni isipokuwa kama kampuni imeshindwa kujiendesha yenyewe ama itajifuta yenyewe, ama kwa oda ya mahakama, mahakama inaweza ikaamrisha kampuni ifilisiwe,” amesema Zitto.

Zitto ameiomba serikali iuondoe muswada huo bungeni , ili kuepusha athari zitakazoweza kusababisha na mabadiliko yatakayoletwa na muswada huo katika sheria.

“Tuliona ni muhimu tueleze haya, wito wetu serikali iachane na muswada huu iuondoe bungeni, na kuonesha muswada kwamba huu una hila wameuleta kwa hati ya dharura Rais John Magufuli amesaini kwa hati ya dharula ili usomwe na ujadiliwe mara ya kwanza ya pili na ya tatu ndani ya siku hizi tatu,” amesema Zitto na kuongeza:

“Tunajua sheria hii inakwenda kuondoa mashirika, wanataka mashirika yafe, ndio hatari ambayo tunayo ndani ya wiki hii Dodoma inakwenda kuwa moja ya wiki nyeusi kwenye nchi hii kama muswada huu usipozuiwa maana yake ni kwamba wiki ijayo tutakuwa na historia mbaya kabisa.”

error: Content is protected !!