January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Kitabu cha Sitta,’ kitabomoa taifa

Mwenyekiti wa Bunge Maalum la Katiba, Samwel Sitta

Spread the love

SASA hakuna katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano – ile iliyokusudiwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ya mwaka 2011.

Kilichovunwa kwa siku 124 mjini Dodoma na ambacho kimetumia zaidi ya Sh. 120 bilioni – fedha za walipa kodi – ni kitabu cha “Samwel John Sitta na wenzake;” lakini siyo Katiba ya nchi.

Kifungu cha 4 (1) (e) cha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kimetaja madhumuni ya kuanzishwa kwa mchakato wa Katiba na kusisitiza, “Katiba Mpya itajengwa kwa njia ya maridhiano.”

Sheria inasema, “Kutawekwa utaratibu ambao utaruhusu wananchi, kushiriki kwa uwazi na mapana katika kutoa maoni na kuyawasilisha.”

Aidha, kifungu cha 4 (1) (j) cha sheria hiyo kinasema, “Kutawekwa utaratibu utakaowezesha kujengwa mwafaka wa kitaifa katika masuala yenye maslahi ya taifa katika mchakato kuhusu Katiba.”

Hayo ndiyo malengo na madhumuni makuu ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, ambayo yalitekelezwa kwa ukamilifu na Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba iliyokuwa chini ya waziri mkuu mstaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Malengo na madhumuni hayo, yametupwa kwa maslahi binafsi ya mwenyekiti wa Bunge Maalum na chama chake – Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Sasa kinachoitwa “Katiba Mpya Inayopendekezwa,” kimeundwa nje ya maoni ya wananchi; kimebadilisha muundo wa serikali na kimehama kutoka kwenye malengo yake makuu na maudhui ya kile ambacho wananchi walitaka na kutarajia.

Kwa njia hii, kuruhusu kitabu cha Sitta kupelekwa kwenye kura ya maoni, ni kukengeuka. Sababu ni hizi:

Kwanza, Katiba Inayopendekezwa, imeacha maoni ya wananchi. Imebeba maoni ya CCM; imebomoa misingi yake mikuu; na imevunja muundo wa Muungano wa Serikali Tatu ambao ulipendekezwa na Tume ya Rais ya Mabadiliko ya Katiba.

Muundo wa Muungano ambao wananchi walitaka, ni kuwapo Jamhuri ya Muungano yenye Shirikisho la Serikali Tatu – Serikali ya Tanganyika, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Muungano.

Lakini Sitta ametupa msingi huu. Amebadilisha mantiki na maudhui. Unapobadilisha mapendekezo ya muundo wa Muungano – kutoka serikali tatu hadi mbili – unakuwa umekosea – kwani hiyo haikuwa kazi ya Bunge Maalum.

Katiba inayopendekezwa imeingiza mambo ya Tanganyika ndani ya Jamhuri ya Muungano; na imebeba mambo yote ya Tanganyika na kuyafanya mambo ya Muungano.

Aidha, Katiba pendekezi imepatikana katikati ya tuhuma za udanganyifu na rushwa. Vilevile, Katiba imepitishwa bila kuwapo akidi; kwa kuwa bado hakuna ushahidi kwamba waliokuwa Saud Arabia kwenye ibada ya Hijja walipiga kura.

Si hivyo tu. Katiba ilipaswa kujengwa kwa njia ya mariadhiano na ushirikishwaji wa wananchi. Hii imeandikwa chini ya ulinzi na misingi ya “wengi wape.”

Kuruhusu dhana ya wengi wape ni kufanya uhuru na haki za watu kuwa mambo ya kupigia kura! Sio sahihi.

Hatari ya wengi wape ni kwamba, waliokuwa wachache leo ndio watakuwa wengi kesho.

Na hilo likitokea, basi waliowengi wa leo; na ambao walikuwa wachache jana, hawatakubali kubaki na katiba hii. Wataikataa.  Ndivyo ilivyokuwa nchini Kenya, Zambia na kwingineko, ambako wale waliojiita “walio wengi” waliamua kulazimisha. Walifanikiwa kupitisha walichokitaka, lakini hakikudumu.

Pale wale waliokuwa wachache huko nyuma – walipokuwa wengi – walifuta yaliyofanyika. Matokeo yake, baadhi ya nchi, ikiwamo Kenya ziliingia katika machafuko.

Pili, miongoni mwa madai ya wananchi yaliyosababisha kuwapo kwa mchakato wa Katiba Mpya, ni pamoja na tuhuma kuhusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kufungwa na chama tawala.

Maoni ya wananchi na taasisi, yalielekeza umuhimu wa kuwapo nchini, chombo huru cha kusimamia uchaguzi. Lengo ni kuzuia taifa kuingia katika machafuko.

Kwa kuzingatia takwa hilo la wananchi, Rasimu ya Jaji Warioba, ilipendekeza kuundwa kwa Tume Huru ya Uchaguzi (NEC). Hii ni kwa kuwa Tume iliyoko sasa, imepoteza uhalali. Ni mtuhumiwa. Haiwezi kusimamia kura ya maoni. Haiaminiki.

Kulazimisha kufanyika kura ya maoni bila kuundwa kwanza tume huru ya uchaguzi, ni kutaka kukanyaga njia ambayo watawala wa Kenya waliamua kupitia.

Ni habati njema, Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu Damian Lubuva, amekiri ukweli huo. Amesema, kwa hali ilivyo sasa, tume yake “haiwezi kuitisha kura ya maoni; na au uchaguzi bila kwanza kuundwa upya daftari la kudumu la wapiga kura.”

Tatu,  Katiba pendekezi imeandikwa chini ya usimamizi wa Andrew Chenge, mmoja wa watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini.

Akiwa mwanasheria mkuu wa serikali (1995-2006), alishauri ununuzi wa rada kwa “bei ya kuruka” kutoka Uingereza. Akatuhumiwa kunufaika na mlungula wa fedha za rada hiyo.

Aliishauri serikali kuridhia kutumika kwa sheria ya Uingereza katika mkataba wa ununuzi wa rada, badala ya sheria za Tanzania.

Alikubali akaunti za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) zishikiliwe jijini London, ili iwapo serikali ya Tanzania ingechelewa au kuishindwa kulipa deni hilo; na mahakama ikaamua kuwa ni lazima ilipe, basi iwe rahisi kwa kampuni ya kutengeneza zana za ulinzi ya British Aerospace (BaE) kuchukua fedha zake.

Ni Chenge kupitia kampuni yake ya Franton Investiment Ltd., anayetuhumiwa kupokea dola za Marekani milioni 1.5 (karibu Sh. 2.5 bilioni) kutoka madalali wa ununuzi wa rada hiyo iliyonunuliwa na serikali mwaka 1999.

Anadaiwa pia kummegea Dk. Idris Rashid, aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), kiasi cha dola za Marekani 600,000 (Sh. 1.2 bilioni) kwa lengo la “kumlainisha.”

Kwa haya mawili na mengine, katiba pendekezi haifai. Chenge hakuwa na hajawa na hadhi wala sifa za kusimamia uandikaji wa katiba hii.

Katiba pendekezi imeshindwa kutengua kitendawili kuwa Zanzibar ni nchi au sehemu ya Jamhuri ya Muungano.

Badala yake, katiba pendekezi imeongeza mgogoro wa kikatiba kati ya Zanzibar na Tanganyika; na Zanzibar na Jamhuri ya Muungano.

Kwa mfano, Rais wa Zanzibar ambaye kwa mujibu wa katiba pendekezi, anafanywa kuwa makamu wa rais wa Muungano, ataapa Zanzibar – kutii katiba ambayo inajitambua kuwa nchi kamili ndani ya Jamhuri ya Muungano.

Baadaye atakula kiapo cha utii kwa Katiba ya Muungano inayoitambua Zanzibar kuwa sehemu ya Jamhuri ya Muungano!

Kwa njia hii, hapatakuwa na katiba.  Kutakuwa na uvunjaji wa katiba. Kuruhusu katiba ya aina hiyo kupelekwa kwa wananchi, ni kutaka kubomoa taifa.

error: Content is protected !!