November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kitabu cha mahabusu chaahirisha kesi ya Mbowe

Spread the love

 

KITABU cha mahabusu cha Kituo kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, kinachoonesha taarifa za Mohammed Abdillah Ling’wenya, kuwekwa katika mahabusu ya kituo hicho, kimesababisha  kesi ndogo inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, iahirishwe. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (Dar es Salaam).

Kesi hiyo ndogo ndani ya kesi kubwa imeahirishwa leo Jumatano, tarehe 10 Novemba 2021 na Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Mawasiliano jijini Dar es Salaam, mbele ya Jaji Joackim Tiganga, hadi kesho Alhamisi tarehe 11 Novemba 2021.

Jaji Tiganga aliahirisha kesi hiyo hadi kesho, ili ajipange kutoa maamuzi madogo juu ya pingamizi la upande wa utetezi dhidi ya  kitabu hicho cha mahabusu, wakitaka kisipokelewe kwa ajili ya utambuzi, kama ilivyoombwa na shahidi wa kwanza wa jamhuri katika kesi hiyo ndogo, Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Arumeru, SP Jumanne Malangahe.

Katika kitabu hiko, kuna taarifa zinazodai Ling’wenya  alifikishwa kituoni hapo tarehe 7 Agosti 2020, akitokea katika Kituo cha Polisi cha Kati Moshi mkoani Kilimanjaro, alikokamatwa kwa kosa la kula njama za kufanya vitendo vya kigaidi, tarehe 5 Agosti mwaka jana.

Mawakili wa utetezi walikipinga kitabu hicho wakidai upande wa jamhuri, wakati unamuongoza  shahidi wake, SP Jumanne haukuweka msingi wa kisheria wa upokelewaji nyaraka hiyo.

Pamoja na shahidi huyo kutothibitisha kitabu hicho kuwa ni cha Kituo cha Polisi cha Kati cha Dar es Salaam, kupitia  mlolongo wa taarifa za mahabusu  na vitu vya kipekee vinavyotihibitisha kuwa kitabu hicho ni cha kituo hicho cha polisi.

Kufuatia pinganizi hilo, upande wa jamhuri waliiomba mahakama hiyo ilitupilie mbali kwa madai kuwa, mawakili wa utetezi walitoa hoja zisizokuwa na msaada wa kisheria.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Abdallah Chavula, alidai hawakubaliani na hoja za mawakili wa utetezi kwa kuwa shahidi huyo ameshindwa kuthibitisha kwamba kitabu hicho ni cha Kituo cha Polisi cha Kati cha Dar es Salaam.

Kuhusu hoja ya mlolongo wa taarifa za mahabusu kutoelezwa katika ushahidi wa SP Jumanne, Wakili Chavula aliipinga akidai, hilo suala linafanywa baada ya usikilizwaji wa shauri na siyo katikati ya shauri.

Wakili Chavula alidai, mawakili wa utetezi hawakutaja mololongo huo unawekwa kwa vigezo gani kisheria ikiwemo kutaja kifungu cha sheria husika na kwamba walichofanya ni kutoa hoja isiyokuwa na msaada wa kisheria.

Kuhusu hoja ya  shahidi huyo kutothibitisha kitabu hicho ni cha Kituo cha Polisi cha Kati cha Dar es Salaam, Wakili Chavula amedai “subject matter yetu ni kilichoingizwa kwenye kielelezo tulichokiomba kwa ajili ya utambuzi wa tarehe 7 Agosti 2020, shahidi anaieleza mahakama kwamba tarehe hiyo alikuwa kwenye chumba cha mashtaka cha kituo hiko,”

“Alifika kwa lengo la kupatiwa mtuhumiwa. Shahidi anasema alipopewa mtuhumiwa aliweka kwenye kielelezo saini kuomba kuondoka na mtuhumiwa. Shahidi akahojiwa atatambua vipi hiko kitabu alichokisiani akasema atakitambua kwa saini yake,”

Wakili Chavula amedai, shahidi aliendelea kusema majina ya mtuhumiwa na  kumbukumbu ya shauri ambayo iko katika kutabu hicho, ambapo taarifa hizo zitakutwa katika taarifa zilizoingizwa tarehe 7 agosti 2020 ndani ya kitabu hiko.

Naye Wakili wa Serikali Mwandamizi, Pius Hilla, amedai  shahidi huyo alithibitisha kuwa kitabu hicho ni Kituo cha Polisi cha Kati cha Dar es Salaam, kwa kusema kuwa alimfikisha Ling’wenya kituoni hapo na kuwa hakuna kituo kingine chenye jina linalofanana na la kituo hiko.

“Shahidi alienda mbele akasema siku ya tarehe 7 Agosti 2020,  alikwenda kwenye chumba cha mashtaka  cha kituo hicho na kumtoa mshtakiwa ambako aliweka saini yake kuonesha alikuwepo hapo. Jaji kwa ushahidi huo ni wazi kuwa alikuwa anazungumzia hiyo nyaraka ni ya kituo gani,” amedai Hilla.

Wakili Hilla ameiomba mahaiama hiyo iyatupe mapingamizi ya utetezi akidai hayana uzito kisheria na kuwa kitabu hiko kipokelewe kwa ajili ya utambuzi kama alivyoomba SP Jumanne.

Kufuatia hoja za mawalili hao wa jamhuri, upande wa utetezi walizijibu ambapo Wakili Jeremiah Mtobesya, amedai uthibitisho unapaswa kufanywa na shahidi na siyo kielelezo chenyewe kama wanavyodai mawakili wa jamhuri.

Wakili Mtobesya amedai, wao hawajapinga taarifa zilizoingizwa katika kitabu hicho  kama ilivyoelezwa na mawakili wa jamhuri, bali wamepinga kitabu chenyewe kuwa hakijathibitishwa na shahidi.

“Nimalizie kwa hoja ya Wakili Hilla,  alisema kuna Kituo cha Polisi Kati cha Dar es Salaam kimoja, lakini kwa bahati mbaya hakuna kitu cha kipekee kinachotambulisha ni cha kituo hicho Polisi.”

“Ni wasilisho letu tangu mwanzo kuwa, hakuna kitu cha kipekee kinachoonesha ni cha Polisi  Kati Dar es Salaam kwa hiyo inakosa miguu ya kusimama ,” amedai Wakili Mtobesya.

Naye Wakili Peter Kibatala, amedai upande wa jamhuri umeshindwa kujenga msingi kuhusu uhusiano wa shahidi na kuelelzo kilichokuwa kimehifadhiwa mahakamani.

Wakili Kibatala amedai, upande wa jamhuri walitakiwa kuiomba mahakama hiyo itoe kielelezo hicho ambacho ilikipokea kama kielelzo namba moja cha shauri dogo la kesi iliyotokana na mapingamizi ya utetezi dhidi ya maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa.

Hivyo upande wa jamhuri unatakiwa uadhibiwe kwa kushindwa kufuata utaratibu huo.e

error: Content is protected !!