May 25, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kitabu cha John Magufuli chafungwa rasmi

Muonekano wa kaburi la Hayati John Magufuli

Spread the love

 

WEWE ni mavumbi na mavumbini utarudi. Ndivyo unaweza kusema, baada ya mwili wa Dk. John Pombe Joseph Magufuli, kulazwa kwenye nyumba yake ya milele, leo Ijumaa tarehe 26 Machi 2021, saa 10:47 jioni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Ni sawa na kusema, kitabu cha Dk. John Pombe Joseph Magufuli, kilichoanza kuandikwa Alhamisi ya tarehe 29 Oktoba mwaka 1959, Chato mkoani Geita, kimehitimishwa eneo hilo hilo kilipoanzia kuandikwa nyumbani kwao.

Kitabu hicho cha maisha ya Hayati Magufuli, aliyekuwa Rais wa tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tangu kuzaliwa hadi mauti yalipomfika na maziko yake, kimetumia siku 22,429 ambazo ni sawa na wiki 3,204 au miaka 61 na miezi minne.

Dk. Magufuli alifariki dunia saa 12:00 jioni ya Jumatano, tarehe 17 Machi 2021, katika Hospitali ya Mzena, Makumbusho mkoani Dar es Salaam, alipokuwa akipatiwa matibabu ya mfumo wa umeme wa moyo wake.

Hayati Magufuli, alizaliwa Chato katika familia ya Mzee Joseph Magufuli na Mama Suzana, akiwa mtoto wa tatu kati ya watoto 12.

Amekuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, kufariki dunia akiwa madarakani. Aliingia madarakani kwa mara ya kwanza tarehe 5 Novemba 2015, akipokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake Jakaya Mrisho Kikwete.

Marais wengine waliomtangulia ambao walifariki baada ya kustaafu ni Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliyefariki tarehe 14 Oktoba 1999 na Benjamin Willium Mkapa, aliyefariki tarehe 24 Julai 2020.

Safari hiyo ya mwisho ya Dk. Magufuli, imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi hiyo, wakiongozwa na Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.

Viongozi wengine ni marais wastaafu Mzee Kikwete, Mzee Mwinyi, Dk. Ali Mohamed Shein, Rais mstaafu wa Zanzibar na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Pia, wamo Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othuman Masoud Othuman, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, Hemed Suleiman Abdulla na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.

Vilio na simanzi, vilitawala kwa wanafamilia na waombolezaji wengine, waliokuwa eneo la makaburi ya familia, ambapo jeneza lenye mwili wa Hayati Magufuli, lilipokuwa likishushwa taratibu ardhini.

Ni tukio ambalo lilikuwa linahitimisha uwepo wa Dk. Magufuli akiwa hai au hata jeneza lenye mwili wake, kwenye sura ya dunia huku ndege vita zikipita angani kutoa heshima.

Maziko hayo yamefanywa kijeshi, yakishuhudia mizinga 21 ikipingwa kutoa heshima za mwisho kwa amri jeshi huyo mkuu, aliyetumikia nafasi hiyo kwa miaka mitano na miezi minne.

Enzi za uhai wake, Hayati Magufuli, amehudumu serikali kwa miaka zaidi ya 25, ikiwemo kuwatumikia wananchi wa Chato kama mbunge wao kwa miaka 20 kuanzia 1995 hadi 2015, kisha akagombea urais na kushinda.

Hayati Magufuli, hadi anafikwa na mauti, ameacha watoto saba ambao ni Suzana, Edna, Mbalu, Joseph, Jesca, Yuden na Jeremiah.

Pia, ameacha Mjane Janeth, ambaye walifunga ndoa takatifu Kanisa Katoliki la Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), mwaka 1989.

Wakati huo, akifunga ndoa, Dk. Magufuli alikuwa mwanafunzi chuoni hapo na aliwahi kunukuliwa akisema “siku niliyooa watu wengi hawakujua…na haimaanishi sikuwa na pesa ya kununua koti au gauni la harusi kwa mke wangu, sikuona kama vitu hivyo ni vya msingi sana.”

“Tulienda hapo kanisani pete tukanunuliwa na Padri, tena zilikuwa za shaba. Padri pia alitununulia soda, nakumbuka mimi nilikunywa pepsi na mke wangu alikunywa mirinda…Baada ya hapo nikaenda zangu lab (maabara) kuendelea na shughuli zangu.”

Simulizi hiyo ya ndoa yake, aliitoa tarehe 1 Novemba 2018, chuoni hapo, wakati akizungumza katika mdahalo wa kutathimini miaka mitatu ya utawala wake, aliokuwa ameingia 5 Novemba 2015.

Kwaheri Dk. John Pombe Joseph Magufuli

error: Content is protected !!