Monday , 27 May 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Kiswahili kimefika kiwango hiki
Makala & Uchambuzi

Kiswahili kimefika kiwango hiki

Mark Zukerberg
Spread the love

KUNA watumiaji wachache wa mtandao maarufu wa facebook wanaofahamu kwamba, mtandao huu unatumia lugha ya Kiswahili kuandaa mikataba ya kulinda taarifa zao za siri zinazoingizwa humo, japo mtandao huo unatumiwa na watu zaidi ya milioni 100 wanaoongea Kiswahili. Anaandika Yusuph Katimba … (endelea).

Haya yamefahamika tarehe 10 Aprili 2018 wakati Mark Zukerberg, mwasisi na Mkurugenzi Mkuu wa mtandao wa facebook, alipowekwa kitimoto na Kamati za Bunge la Marekani za sheria na biashara zinazosimamia masuala ya haki za watumiaji wa huduma. 

Katika mahojiano yaliyofanyika kwa siku mbili mfululizo kuanzia 10 Aprili 2018, Seneta wa Louisiana,John Kennedy, alimwambia maneno haya Zukerberg:

“Nataka kupendekeza kwamba, uende nyumbani na kumwambia mwanasheria wako unayemlipa Dola 1,200 kwa saa kuwa, mikataba hiyo inapaswa kuandikwa kwa Kiingereza na sio Kiswahili, kusudi kila Mmarekani wa kawaida aweze kuilewa.” 

Kauli hii ilizua hasira kutoka kona mbalimbali duniani, Seneta Kennedy akituhumiwa kwa ubaguzi wa lugha zisizo za Kiingereza, na hasa ubaguzi dhidi ya Waafrika wengi wanaotumia lugha ya Kiswahili.

Mtandao wa facebook unatumiwa duniani nzima, kiasi watumiaji wa Kiswahili wapatao milioni 100 hawawezi kuongelea intaneti bila kuutaja.

Japo watumiaji hawa wana kitovu chao katika Afrika Mashariki, wamesambaa duniani kote mpaka Oman, Afrika Kusini, Asia, Ulaya na ndani ya Amerika kwenyewe.

Kwa mujibu wa Profesa Ali Mazrui, lugha ya Kiswahili imegeuka lugha ya kimataifa ndani na nje ya Afrika kwa sababu ya kurithi misamiati yake kutoka katika vyanzo vitatu, yaani, lugha asilia za kibantu, mapokeo ya Mashariki kupitia Dini ya Kiislamu pamoja na wafanyabiashara kutoka Bara la Asia na mapokeo ya Magharibi kupitia Dini ya Kikristo pamoja na wakoloni wa kizungu. Kwa ufupi, Kiswahili ni kama lugha ya biashara ndani ya eneo kubwa ndani na nje ya Afrika.

Kwa siku mbili mfululizo, Zukerberg alihudhuria mahojiano kati yake na wabunge wa Marekani, kuhusu tuhuma kwamba kampuni moja ya Kompyuta kutoka Uingereza, iitwayo Cambridge Analytica, ilichota na kutumia taarifa binafsi za wateja waliojisajili katika mtandao wa facebook, lakini bila kuomba ridhaa ya watumiaji hao, na kuzitumia kumfanyia kampeni Rais Donald Trump kwenye uchaguzi mkuu wa 2016.

Mbali na kuingilia faragha ya watumiaji wa facebook bila ridhaa yao, kampuni ya Cambridge Analytica inatuhumiwa kutumia taarifa hizo kusambaza taarifa feki mtandaoni kwa lengo la kumfanya Trump ashinde.

Tuhuma kama hizo zimekuwa zinaukabili uongozi wa mtandao wa facebook kutoka nje ya Amerika pia, na hasa katika mataifa ambayo hayana ufundi wa kudhibiti taarifa zinazoeza kusababisha vurugu na vifo zinazosambazwa na watumiaji wenye nia ovu kupitia mtandao huu.

Kwa mfano, inaaminika kuwa, nchini Kenya mitandao ya facebook na whatsApp ilitumika kusambaza habari za uongo wakati wa uchaguzi uliokuwa na ushindani mkubwa.

Na kwamba, hatua hiyo ilichangia katika kuchochea tukio la mauaji ya watu zaidi ya 100. Kampuni ya Cambridge Analytica inatuhumiwa kufanya jambo kama hilo huko Nigeria.

Huko nje ya Afrika, tatizo la usambazaji wa taarifa za uongo mitandaoni kupitia mtandao wa facebook na mitandao mingine, ni kubwa.

Tayari mtandao wa facebook unalaumiwa kusababisha chuki Waislamu wa Rohingya huko Myanmar. Katika nchi ya Ufilipino Rais Rodrigo Duterte anatuhumiwa kuutumia mtandao wa facebook kuwanyamazisha wapinzani wake.

Aidha, kuna tuhuma kuwa, facebook ilitumika kusambaza taarifa za uongo zilizochangia katika kuwafanya wapiga kura wa Uingereza kupiga kura ya kujitoa katika Jumuiya ya Ulaya kwa sababu ya kufuata mkumbo tu.

Ni katika mazingira haya, Mkurugenzi Zukerberg aliwekwa kiti moto, huku maseneta wakimwambia kuwa kama hawawezi kusimamia biashara yao vizuri Bunge litalazimika kuwasaidia kuisimia biashara hiyo kwa kutunga sheria mahususi kwa ajili ya kuratibu kazi za mtandao wa facebook.

Mwisho wa mahojiano, Seneta Long alisikika akisema, “Wewe ndiye mtu unayepaswa kuziba mianya ya matumizi mabaya ya mtandao wenu, na sio sisi. Unapaswa kuliokoa jahazi lako.”

Naye Seneta akahitimisha mahojiano kwa kusema, “Sitaki kupiga kura ya kutunga sheria ya kusimamia shughuli za facebook kadiri suala la kulinda haki ya faragha ya watumiaji linavyohusika, lakini Mungu akipenda nitafanya hivyo.”

Naye Zukerberg aliwaahidi wabunge wa Marekani kwamba atafanya kila juhudi kuhakikisha kuwa, taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao wake zinalindwa na kwamba mtandao huo unatumiwa vizuri.

“Tunao wajibu wa kulinda taarifa binafsi za watumiaji wa mtandao wetu, na kama tunashindwa hatustahili kuwahudumia,” alisema Zukerberg.

Jukumu la kulinda taarifa binafsi zinazopatikana kupitia mawasiliano binafsi yanayohusisha pande mbili, kati ya wakala na bosi wake, sio la sheria za Marekani pekee.  Hata sheria za Tanzania zinalitambua.

Taarifa binafsi zinazotolewa na mwajiriwa kwa mwajiri wake, mwanafunzi kwa mwalimu wake, mgonjwa na daktari au taarifa zinazotolewa na mshitakiwa kwa wakili wake, ni taarifa za siri. Zinatolewa katika mazingira ya kuaminiana.

Katika mazingira haya, mtoa taarifa anaitwa mtu wa upande wa kwanza (first party); mpokea taarifa anaitwa mtu wa upande wa pili (second party); na watu baki ambao hawakuhusika moja kwa moja katika muamala wa makabidhiano ya taarifa binafsi wanaitwa watu walio katika upande wa tatu (third party).

 Lakini, watu walio katika upande wa tatu wanagawanyika katika makundi mawili. Kwa upande mmoja, kuna watu walio katika upande wa tatu na ambao, kwa njia ya mzunguko, wanayo ruhusa ya kuziona na kuzifanyia kazi taarifa za siri, japo hawakushiriki katika muala wa makabidhiano yake.

Kwa mfano, bila kuomba upya ridhaa ya mgonjwa, mtaalam wa maabara anayo nafasi ya kuziona na kuzifanyia kazi taarifa za mgonjwa zinazotolewa kwa daktari.

Na kwa upande mwingine, kuna watu walio katika upande wa tatu na ambao, hata kwa njia ya mzunguko, hawana ruhusa ya kuziona na kuzifanyia kazi taarifa za siri, mpaka waombe upya na kupatiwa kibali au ridhaa ya mtoa taarifa wa kwanza.

Bunge la Marekani lilitaka kujua ni kwa kiasi gani uongozi wa mtandao wa facebook unasimamia sheria za aina hii.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Rais Samia muonee huruma Dk. Phissoo

Spread the loveRAIS wangu mama Samia, wiki iliyopita baada ya kuwa nimekuandikia...

Habari MchanganyikoMakala & Uchambuzi

GGML inavyookoa walemavu dhidi ya dhana potofu

Spread the loveMKOA wa Geita ni mmoja wa mikoa ya Kanda ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Miaka 63 ya Uhuru bila katiba ya wananchi

Spread the loveWAFUASI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanaharakati...

AfyaMakala & Uchambuzi

Uongo, uzushi, tiba ya matende, ngiri maji

Spread the loveKUNA uongo na uzushi katika jamii kuhusu wanaume, wanawake na...

error: Content is protected !!