May 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kisima cha mwaka 1989 chafufuliwa Dodoma, mkandarasi apewa siku 60

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maji nchini Tanzania, Mhandisi Nadhifa Kemikimba akizindua kisima

Spread the love

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Maji nchini Tanzania, Mhandisi Nadhifa Kemikimba, ametoa siku 60 kwa mkandarasi SUMA JKT anayejenga tanki la maji eneo Buigiri wilayani Chamwino jijini Dodoma kuhakikisha anakamilisha kazi hiyo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Pia, ameipongeza Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Mji wa Dodoma (DUWASA), kwa kufufua kisima cha maji kilichojengwa mwaka 1989 eneo la Nzuguni kilichoanza kutoa maji.

Kuhusu ujenzi wa tanki hilo la maji lenye ujazo wa wa lita milioni 2.5,  linajengwa kwa gharama ya Sh.998 milioni na linatarajiwa kuhudumia wakazi wa Chamwino Ikulu,Hospitali ya Uhuru na Buigiri.

Akizungumza akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua maendeleo ya miradi mbalimbali ya maji jana Jumapili tarehe 3 Januari 2021, Mhandisi Nadhifa alisema, tanki hilo lilitakiwa lijengwe Septemba 2020 lakini limechelewa kukamilika.

“Tumekubaliana na mkandarasi kuwa tenki hili likamilike ndani ya miezi miwili, ili kuharakisha kazi hii, menejimenti ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mjini Dodoma (DUWASA) fuatilieni kazi hii kila siku ili mradi ukamilike kwa wakati,” aliagiza Mhandisi Nadhifa.

Mbali na mradi huo, Mhandisi Nadhifa ametembelea eneo la Ihumwa panapochimbwa visima, ametembelea eneo la Nzughuni kunapofufuliwa kisima ambapo alisema ameridhishwa na utendaji kazi wa DUWASA.

“Hapa nimeridhishwa na menejimenti ya DUWASA, wamefanya jitihada kubwa ya kuhakikisha wananchi wanapata maji, kazi inayofanyika hapa ni kufufua visima ambavyo vilichimbwa zamani ni ubunifu mkubwa, hongereni sana,” alipongeza.

Naibu katibu mkuu huyo aliitaka DUWASA kuongeza kasi ya kukamilisha ufufuaji na uchimbaji wa visima hivyo ili wananchi wa Jiji hilo la Dodoma ambapo ni makao makuu ya nchi waondokane na usumbufu wa kukosa huduma hiyo muhimu.

Akizungumza katika eneo hilo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa DUWASA, Aron Joseph alisema, dhamira waliyonayo ni kuvifufua visima vya zamani ili visaidie kutoa huduma na mpaka sasa wameshavitambua visima 11 vilivyopo katikati ya mji.

“Kisima hiki kilikuwepo tangu mwaka 1989 lakini kutokana na changamoto mbalimbali kilitelekezwa, dhamira yetu ni kuvitambua na kuvifufua visima hivi ili viweze kusaidia kutoa huduma ya maji kwa wananchi na hivyo kupunguza upungufu wa maji uliopo,” alisema Joseph.

Joseph alisema, matokeo ya majaribio ya kisima hicho, yameonyesha  kitakuwa kina uwezo wa kutoa lita 8000 kwa saa na kwa siku lita 192,000.

error: Content is protected !!