January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kishowa aitoa serikali mafichoni

Spread the love

DAKTARI Leonard Chamuriho ambaye ni Katibu Mkuu wa Idara ya Uchukuzi katika Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amesema, uchunguzi kuhusu kesi ya uagizwaji wa mabehewa 274 yaliyoingizwa nchini, bado haujafika tamati. Anaandika Regina Mkonde.

Dk. Chamuriho ametoa ufafanuzi huo ikiwa ni siku moja tu baada ya Jeska Kishowa Kafulila, Mbunge Viti Maalum (Chadema) kusimamishwa vikao viwili mfululizo kuanzia jana baada ya kuishambulia serikali kuhusu uingizwaji wa mabehewa hayo.

Kishowa alisimamishwa na Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Bunge kwa madai ya kushindwa kutoa uthibitisho juu ya madai yake kuwa Harrison Mwakyembe ambaye alikuwa Waziri wa Uchukuzi karika serikali iliyopita, alitumia Sh. 238 bilioni kununua mabehewa mabovu.

Dk. Chamuriho amesema, uchunguzi unaoendelea na kwamba hakuna ushahidi wa kutosha hadi sasa.

“Shauri la kwanza linahusu uongozi wa TRL kukiuka sheria ya manunuzi ya Umma ya 21 pamoja na kanuni zake mwaka 2014, kuhusiana na manunuzi ya mabehewa 25 ya aina ya Ballast Hopper Bogie Wagons kutoka Kampuni ya Hindustan Engineering and Industries LTD,” amesema Chamuriho na kuongeza;

“Shauri hili lilikuwa linachunguzwa na Takukuru, uchunguzi huo umekamilika na faili limepelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka ya Jinai (DPP).”

Mabehewa hayo 274 yalinunuliwa na Shirika la Reli Tanzania (TRL) kutoka Kampuni ya Hindustan Engineering and Industries LTD mwaka 2015.

Hoja hiyo iliibuliwa kwa mara ya kwanza bungeni na Kishowa tarehe 01 Februari mwaka huu katika mkutano wa pili wa Bunge la 11.

Hoja hiyo iliibuliwa na Kishowa (Viti Maalum) wakati akichangia Hotuba ya Waziri wa Fedha na Mipango kuhusu mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2016/2017.

Kuhusu mashitaka ya ununuzi wa mabehewa feki 274, Dk. Chamuriho amesema uchunguzi wake bado unaendelea na umegawika sehemu tatu.

“Uchunguzi umegawanyika sehemu tatu, mabehewa ya mizigo yaliyofunikwa 174, mabehewa ya mafuta 50 na mabehewa ya kubebea makontena 50,” amesema.

Hata hivyo, Dk. Chamuriho ameshindwa kutoa maelezo kuhusu idadi ya mabehewa yaliyoharibika na kudai kuwa, sheria ya uchunguzi haimruhusu kuongea chochote kuhusu hilo.

“Kama nilivyosema awali, siwezi nikatolea ufafanuzi suala hili sababu lipo nje ya uwezo wangu, nikieleza sasa nitakuwa nakiuka sheria na taratibu za uchunguzi. Kilichonileta ni kutoa taarifa kwamba, uchunguzi bado unaendelea ukikamilika kila kitu kitajulikana,” ameeleza.

error: Content is protected !!