July 1, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kishoa: Nikichaguliwa Iramba itanyooka

Spread the love

MGOMBEA ubunge Jimbo la Iramba Magharibi kupitia Chadema, Jecsa Kishoa amesema akichaguliwa kuongoza jimbo hilo, Halmashauri ya Iramba itanyooka. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Amesema, kukomaa kwa vitendo vya rushwa na ufisadi kwenye halmashauri hiyo kunatokana na kutokuwepo kwa mtu makini aliye na uchungu na fedha za umma.

Hata hivyo ameeleza kuwa alianza mapambano dhidi ya wanaofanya ufisadi na kukwamisha maendeleo katika halmashauri hiyo na kuahidi kwamba, iwapo atachaguliwa, atapeleka hoja bungeni na kutoa ushahidi katika vyombo vya sheria ili hatua ziweze kuchukuliwa.

Kishoa ambaye mpinzani wake mkubwa ni mbunge wa jimbo hilo na Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ametoa kauli hiyo leo, wakati akizungumza na MwanaHALISI Online kuhusu vipaumbele ambavyo atavifanyia kazi iwapo atachaguliwa na wananchi kuwa mbunge wa jimbo hilo.

“Kipaumbele cha kwanza ni kupambana na ufisadi unaofanywa na watendaji wa halmashauri. Mabilioni ya fedha yameliwa na mkurugenzi, badala kuwajibishwa amehamishwa ,” amesema Kishoa.

Kuhusu kipaumbele cha pili Kishoa amesema atatenga asilimia 30 ya mshahara wake ili kusaidia mahitaji binafsi ya wanafunzi wasio jiweza.

Amesema “kipaumbele change cha tatu ni kushughulikia tatizo la maji. Kwa muda mrefu wananchi wa Iramba wanatumia maji ambayo pia yanatumiwa na mifugo kama Mbuzi, Punda na Ng’ombe. Nitaisumbua serikali mpaka itatue changamoto hii.”

Pia, amesema kipaumbe chake cha nne ni kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata nyezo za kazi mfano nguzo za kuzuia maporomoko ya udongo, hewa na kushawishi serikali kutunga sheria ya kulinda wachimbaji wadogo.

“Kipaumbele cha tano ni kuhakikisha reli iweze kufika Misigiri ili kusaidia wakulima, wafugaji na wafanyabiashara kusafirisha bidhaa zao,” amesema Kishoa.

error: Content is protected !!