August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kisasi cha Dk. Magufuli CCM

Spread the love

MKUTANO Mkuu Maalum wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) utakaofanyika tarehe 23 Julai mwaka huu, haufurahiwi na baadhi ya makada wa chama hicho, anaandika Charles William.

Kundi lililomtenga kabla na wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ndilo linalokwenda Dodoma kwenye mkutano wa makabidhiano ya uenyekiti huku likiwa na kinyongo.

Makabidhiano ya uenyekiti wa CCM ni kutoka kwa Dk. Jakaya Kikwete (mwenyekiti wa sasa wa chama hicho) kwenda kwa Dk. John Magufuli, Rais wa Tanzania.

Ratiba ilivyo, Mjini Dodoma tarehe 21 kutafanyika Kikao cha Kamati Kuu ya CCM, tarehe 22 kitafanyika Kikao cha Halmshauri Kuu ya CCM ambapo tarehe 23 Julai utafanyika mkutano Mkuu Maalum kwa ajili ya kumkabidhi chama Dk. Magufuli.

Katika makabidhiano hao lipo kundi ndani ya CCM linahofia Dk. Magufuli kukabidhiwa uenyekiti wa chama hicho kwamba ‘ataanza kuwasulubu.’

Kundi hilo linajulikana kutokana na kauli kadhaa zilizowahi kutolewa na Dk. Magufuli wakati wa kampeni za Uchaguzi Mkuu wa tarehe 25 Oktoba mwaka jana.

Katika siku za hivi karibuni, vyombo vya habari vilieleza kuwepo kwa kundi mawili ndani ya CCM, mmoja likitaka Dk. Kikwete kukabidhi uenyekiti wa chama hicho kwa Dk. Magufuli mwaka huu lingine likipigia chapuo mpaka mwakani.

Mtoa habari wetu ndani ya CCM anaeleza kuwa, kundi lililo na hofu na Dk. Magufuli ni lile lililoonekana kumpuuza wakati wa kampeni za uchaguzi jambo ambalo mwenyewe (Magufuli) analijua.

“Kuna kundi ambalo kwa sasa halina amani, lilidhani linaweza kuendelea kuwepo mpaka mwakani lakini hatua hii inayokwenda kufanikiwa inawanyima raha,” ameeleza na kuongeza;

“Dk. Magufuli anazo taarifa za watu ama makada wa CCM ambao kwenye uchaguzi mkuu walikuwa tofauti nao.

“Hawa wanajua misimamo yake kwa muda mrefu, hawakutaka hata awe rais wa nchi. Wanayo hofu kwamba anaweza kaunza nao,” amesema.

Awali Dk. Magufuli aliwahi kumwambia Dk. Kikwete (mwenyekiti wa sasa) kwamba, akiwa kama mwenyekiti wa chama hicho, anazungukwa na wanafiki.

“Unazungukwa na wanafiki na watu ambao ulidhani watakusaidia katika chama lakini wamekuangusha.”

Dk. Magufuli alimwambia maneno hao Dk. Kikwete tarehe 30 Oktoba mwaka jana wakati Jaji Mstaafu Damian Lubuva, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (ZEC) akimkabidhi cheti cha ushindi wa mbio za urais.

Kabla ya kauli hiyo, Dk. Magufuli kwenye mikutano yake ya kampeni alikuwa akionya makada wa chama hicho ambao ‘mchana wanakuwa CCM na usiku wanahamia Ukawa.’

Mtoa taarifa anadokeza kuwa “kundi hilo lipo na linajulikana. Kitu kibaya zaidi ni pale walipoendelea na harakati za kutaka kuzuia Magufuli asikabidhiwe uenyekiti.”

Anaeleza kuwa, kwa namna alivyo Dk. Magufuli, watu hao hatowaacha na kwamba, atakuwa akifanya kusafisha chama kama alivyofanya na anavyofanya ndani ya serikali yake.

Mtoa taarifa anasema, ndani ya chama hicho kulikuwa na msuguano wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu na kwamba, moja ya mambo yanayofanyika kwa sasa ni kuhakikisha viongozi waliopo sasa wanaondolewa kwenye nafasi zao na kupelekwa serikalini.

“Watu wanajiuliza mbona makada wa CCM ndio wanaingizwa serikalini? Jibu ni rahisi kwamba, mkuu ana lengo la kutaka kuwa na timu mpya ndani ya chama lakini pia timu mpya ndani ya serikali.

“Hata hawa walio na vyeo vya juu baadaye watapata nafasi zingine ndani ya serikali na ndani ya chama utaona sura zingine kabisa. Anafuta yaliyopita anatengeneza mapya,” kimeeleza chanzo hicho.

Amesema kuwa, watu wanaotarajiwa kuwa majeruhi wa kwanza baada ya Dk. Magufuli kukabidhiwa chama ni wale aliowataja kuwa wanafiki ama wasaliti na kuwa, baadhi yao anayo majina yao.

error: Content is protected !!