SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, ametoa maagizo kwa walinzi wa Bunge hilo, kutowaruhusu wabunge wanaovaa vibaya kuingia bungeni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).
Ni baada ya leo Jumanne, tarehe 1 Juni 2021, kumtoa ndani ya ukumbi wa Bunge, mbunge wa Momba (CCM), Condester Sichwale, kutokana na kuvaa mavazi yasiyo ya kibunge.
Ilikuwa baada ya kumalizika kwa kipindi cha maswali na majibu, akasimama mbunge wa Nyang’wale (CCM), Hussein Amar kuomba mwongozo.
“Spika nasimama kwa kanuni ya 170 inayohusu mavazi ya staha kwa wabunge, kanuni imeeleza wazi kuhusu mavazi hayo na kwa akina dada lakini humu ndani kuna wabunge wamevaa nguo ambazo hazina staha,” amesema Amar.

Baada ya kutoa mwongozo huo, Spika Ndugai alimwomba atoe mfano wa mbunge ambaye hajavaa vizuri.
Mbunge huyo alisimama na kusema “mbunge huyo yuko hapo katika mkono wangu wa kulia, amevalia tisheti lakini naomba umuite mbele hapo uone suruali aliyovaa namna ilivyobana, amevaa miwani.”
Mara baada ya kumaliza kumtaja, Spika Ndugai alisimama na kumtaka mbunge huyo asimame na aondoke ndani ya ukumbi ili akavae mavazi yenye staha.
Spika Ndugai ameagiza askari wote katika milango ya kuingia bungeni wawe makini wasiruhusu wabunge kuingia wakiwa wamevaa mavazi yaliyokatazwa.
Ni kweli nguo alizovaa hazina staha? Spika unaishi nchi gani na karne gani? Hiyo nguo ni ya kawaida kabisa wala haina dosari. Mumehudhuria gwaride la majeshi na mumeona askari wetu wa kike wanavyovaa suruali wakati wakipita mbele ya Rais?