May 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kisa koroka: Bila barakoa huingii soko la sabasaba Dodoma

Spread the love

 

UONGOZI wa Soko la Sabasaba jijini Dodoma, umepiga marufuku mtu yeyote kuingia ndani ya soko hilo bila kuvaa barakoa. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mkakati huo umeandaliwa ni kuhakikisha wanawakinga wananchi wanaofika sokoni hapo ikiwemo wauzaji na maambukizi ya ugonjwa wa korona (UVIKO-19).

Maji tiririka pamoja na sababu yamewekwa maeneo mbalimbali ya soko hilo kuhakikisha wananawa mikono.

Leo Jumatatu, tarehe 9 Agosti 2021, akizungumza na vyombo vya habari sokoni hapo, Kaimu mwenyekiti wa soko hilo, Adam Kombo amesema, hatua hiyo inafanyika baada ya kukubaliana kwa pamoja umuhimu wa kuvaa barakoa pindi mtu anapoingia sokoni.

“Tumeweka utaratibu wa kuhakikisha watu wote ambao wanaingia katika soko la sabasaba wanavaa barakoa,” amesema Kombo.

“Tumeweka maji tiririka kila mlango wa kuingilia, tumeweka vitakasa mikono na kila mlango kuna watu ambao wanauza barakoa na zaidi ya yote kuna mgambo kila mlango ambaye kazi yake kubwa ni kuwazuia watu wasiokuwa na barakoa wasiingie ndani ya soko,” amesisitiza

“Hatuwezi kuwa wapole kwa jambo hili ni bora tuwe wakali watu watuchumkie kuliko kuwa wapole na kutafuta sifa wakati wapo watu wanaangamia,” amesema Kombo.

Kwa upande wake, afisa afya Kata ya Viwandani, Fausta Kibiti amesema kwa kutekeleza maagizo ya mkuu wa mkoa wa Dodoma, Antony Mtaka ya kutaka watoa huduma na wanaopatiwa huduma kuvaa barakoa sasa wanalitekeleza kwa vitendo.

“Uongozi wa ofisi ya afya kata ya Viwandani kwa kushirikiana na uongozi wa soko la sabasaba, tunaendesha oparesheni ya kuwataka watu wote wavae barakoa.”

“Tumekuwa na oparesheni kwa wale ambao wanauza mitumba kwa kuwataka wavae barakoa na wanaokaidi wanatolewa na Mgambo ndani ya soko,” amesema Fausta.

“Tunatoa elimu juu ya umuhimu wa kuvaa barakoa na ikumbukwe kuwa katika magulio kuna msogamano mkubwa ambao ni hatari kwa afya ya watoa huduma na wapokea huduma,” amesema

Baadhi ya wafanyabiashara na wateja katika soko hilo kwa nyakati tofauti wamesema, utaratibu wa kuvaa barakoa ni mzuri kwani ni kwa faida ya mtu mmoja mmoja na kuzuia maambukizi kwa mtu mwingine.

“Tunaona utaratibu huu wa kuvaa barakoa na kunawa mikono ni utaratibu ambao unafaa kuzingatiwa bila hata kulazimishwa kwani kwa sasa hali ya ugonjwa ni mbaya na ukizingatia hii mikusanyiko ni lazima kuvaa barakoa” wamesema wafanyabiashara.

error: Content is protected !!