January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kipindupindu chaingia Dodoma

Spread the love

WATU wawili wamefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Kipindupindu mkoani wilayani Kongwa, Dodoma. Anaandika Dany Tibason, Kongwa … (endelea).

Kauli hiyo ilitolewa jana mjini hapa na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Ezekiel Mpuya. Dk. Mpuya amesema hivi karibuni walipokea mgonjwa mmoja wa kipindupindu kutoka katika kijiji cha Mkoka kata ya Mkoka wilayani Kongwa.

“Hapo kulikuwa na familia moja iliyokuwa mkoa wa Morogoro kwenye eneo ambalo linasadikiwa kuwa na ugonjwa wa kipindupindu, alisafiri kuja eneo la Mkoka bila ya wao kufahamu mtoto alianza kuharisha.

“Lakini alipopelekwa kwenye kituo cha afya cha Mkoka na kuchukuliwa vipimo walibaini kwamba ni ugonjwa wa kipindupindu,” amesema.

Aidha, amesema hadi juzi kulikuwa na wagonjwa saba kwenye kituo hicho ambapo wawili walifariki dunia.

Hata hivyo, amesema katika kijiji hicho cha Mkoka kuna mwanakijiji mmoja naye alisafiri kuja Manispaa ya Dodoma ambapo alionekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.

“Alipoona dalili hizo aliamua kwenda kwenye kituo cha Afya cha Makole na kuchukuliwa vipimo, ingawa vipimo vimeonyesha kuwa hana dalili za kuhara lakini sisi tunamashaka na tunaendelea kumuhudumia,” amesema.

Aidha, amewaasa wananchi kuwa waangalifu ikiwa ni pamoja na kuchukua tahadhari kwa kuwa ugonjwa wa kipindupindu unatokana na kula kinyesi.

“Wanatakiwa kunawa mikono na sabuni wanapotoka chooni na kabla ya kula, na vyakula wanavyokula viwe visafi,” amesema.

Amesema walipotembelea katika kijiji cha Mkoka waligundua kuwa wakazi wengi wa eneo hilo hawana vyoo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Donan Mmbano amesema mpaka sasa ni mikoa mitano ndiyo iliyoathirika na Ugonjwa wa Kipindupindu.

Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Dar es Salaam, Dodoma, Kilimanjaro, Iringa na Morogoro.

error: Content is protected !!