December 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kinyang’anyiro cha Urais Chadema: Nyalandu kumkabili Lissu

Lazaro Nyalandu

Spread the love

ALIYEKUWA mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu, ameanza kupata upinzani mkali katika mbio zake za kutaka kuwania urais, kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Ni baada ya Lazaro Nyalandu, mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kati, kutajwa kuungana na makada wengine kuomba ridhaa ya kupeperusha bendera ya chama hicho, katika uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu.

Mbali na Lissu, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Chadema (Bara), mwingine aliyejitokeza katika kinyang’anyiro hicho, ni Mchungaji Peter Msigwa, mbunge wa Iringa Mjini na Dk. Maryrose Majinge.

John Mnyika, katibu mkuu wa Chadema, alieleza kuwa “utiaji nia ulianza tarehe 3 hadi 15 Juni 2020.”

MwanaHALISI ONLINE limedokezwa na watu wa karibu na Nyalandu, kwamba atajitosa kuwania nafasi hiyo.

“Nyalandu anajitokeza kugombea, sijajua ni lini atatangaza nia, lakini anajipanga kabla ya tarehe 15 Juni 2020 atatangaza nia,” kimedokeza chanzo hicho.

Mwandishi wa taarifa hizi, ameshindwa kumpata Nyalandu ili kuzungumzia suala hilo kwa kina na kujua hasa ni lini atapeleka barua yake ya kutia nia kwa katibu mkuu.

Tundu Lissu, Makamu Mwenyekiti wa Chadema

Nyalandu aliyekuwa mbunge wa Singida Kaskazini kati ya mwaka mwaka 2000 hadi tarehe 30 Oktoba 2017 na kujiunga na Chadema.

Nyalandu alizaliwa tarehe 18 Agosti 1970, mkoani Singida, ameshika nafasi mbalimbali za uongozi, akiwemo waziri wa maliasili na utalii.

Alipata elimu ya msingi katika shule za Msingi Pohama na Mrumba zilizoko kijijini kwao Singida na kuhitimu mwaka 1987.

Aliendelea na masomo ya kidato cha kwanza mpaka cha nne katika Shule ya Sekondari Kibaha mkoani Pwani (1988 –1991) na alifaulu vizuri na kujiunga na Shule ya Sekondari Ilboru ambako alisoma kidato cha tano na sita.

Wakati akiwa mwanafunzi wa Sekondari (1991–1993) Nyalandu, alikuwa kiongozi wa juu wa ushirika wa Kikristo wa Wanafunzi Tanzania (Ukwata) na baadaye alikuwa miongoni mwa vijana wa Kitanzania walioteuliwa kuzuru jiji la Rio De Janeiro, Brazil na kushuhudia mkutano wa mazingira mwaka 1993.

Nyalandu alipata elimu yake ya Chuo Kikuu nchini Marekani ambako alihitimu Shahada ya kwanza ya Sanaa katika Usimamizi wa Biashara (BBA) mwaka 1997 katika Chuo Kikuu cha Wartburg.

Kabla ya hapo, alikuwa amepata Shahada ya Biashara ya Kimataifa kutoka Chuo Kikuu cha Wardorf nchini humo.

Dk. Maryrose Majinge, kada wa Chadema aliyetangaza nia ya kuwania Urais kupitia chama hicho

Mwanasiasa huyo, ana Shahada ya Uzamili aliyoipata kwa njia ya utafiti kutoka Chuo Kikuu cha Buckingham, Uingereza akifuzu katika masuala ya Ushirikiano wa Kimataifa na Diplomasia.

Baada ya kuhitimu masomo yake ughaibuni, Nyalandu alianza kazi huko huko Marekani katika Benki ya North West, akifanya kazi katika kitengo cha operesheni za kibenki kati ya mwaka 1998 hadi 1999.

Aliporejea nchini Tanzania alifanikiwa kuwa sehemu ya washauri wa mke wa aliyekuwa Rais Benjamin Mkapa, Mama Anna Mkapa, katika uendeshaji wa taasisi ya Mfuko wa Fursa Sawa kwa Wote (EOTF).

Ushauri wa timu yake ulisaidia taasisi hiyo kupata misaada mingi kutoka nchi za Ulaya, Marekani, China na nyinginezo.

Alikuwa pia anamsaidia mama huyo katika uandishi wa hotuba zake, pale alipokuwa na majukumu makubwa ya kitaifa na kimataifa.

Nyalandu amemwoa mrembo wa Tanzania mwaka 2004 ‘Miss Tanzania,’ Faraja Kotta na wana watoto wawili, Sarah na Christopher.

Alikuwa mstari wa mbele katika kusaidia Jamii katika masuala ya Elimu na Afya, ambapo alikuwa Mwanzilishi Mwenza  wa Shirika la STEMM ambalo limesomesha wanafunzi zaidi ya 10,000 kwa kuwalipia ada za Sekondari, na baadhi  yao kuwapa ufadhili katika Vyuo Vikuu.

Aidha, alisaidia kuwapeleka Nje ya nchi kwa matibabu watoto walionusurika katika ajali ya busi la Lucky Vicent iliyotokea Mei 2017 na kusababisha vifo vya wanafunzi na walimu zaidi ya 30.

error: Content is protected !!