June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kinondoni kupekuwa wasio na makaro ya majitaka

Spread the love

HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni imesema kuwa, ifikapo Juni mwaka huu itawachukulia hatua za kisheria wenye nyumba wasiojenga makaro ya kuhifadhia majitaka. Anaandika Regina Mkonde.

Akizungumza na MwanaHALISI Online jijini Dar es salaam leo, Sebastian Mhowera Ofisa Uhusiano Manispaa ya Kinondoni, amesema kuwa toka mwaka jana halmashauri ilitoa waraka kwa wenyenyumba wasio na makaro kujenga.

“Wenyenyumba hasa wanaozunguka mradi wa DART wasiokuwa na makaro ya kuhifadhia majitaka na kinyesi, wahakikishe wanajenga ili kupunguza umwagaji holela majitaka na kinyesi,” amesema Mhowera.

Mhowera amesema kuwa, Kinondoni inaongoza kwa kuwa na nyumba ziziso na makaro ya majitaka hasa zilizo katikati ya wilaya na upungufu wa miundombinu ya kutosha ya kusafirishia maji hayo.

“Serikali imetoa agizo ifikapo Juni mwaka huu wasiokuwa na makaro kujenga, kama hawana maeneo ya kutosha kuvunja baadhi ya vyumba ili wajenge. Wasiofanya hivyo watachukuliwa hatua za kisheria,”

Jiji la Dar es salaam linakabiliwa na changamoto ya upungufu wa miundombinu ya majitaka na kusababisha umwagaji holela wa maji taka hasa wakati wa mvua.

“Baadhi ya wananchi hutumia kipindi cha mvua kufungulia majitaka na kinyesi na kuyaelekezea kwenye mifereji iliyojengwa kwa lengo la kusafirishia maji taka,”ameongeza.

Mhowera amesema, wananchi wa Dar es salaam wanaongoza kutupa taka ngumu kwenye mitaro ya maji na sehemu zisizo rasmi na maji taka yenye kinyesi kwenye mito, mitaro na mifereji.

“Serikali inapoteza fedha nyingi kuchimba mito, mifereji na mitaro ili kuongeza kina, ikiwa na lengo la kupunguza mafuriko na magonjwa ya milipuko inayosababishwa na maji taka kutuama muda mrefu,” amesema.

Kwa upande wa ugonjwa wa kipindupindu, amesema hakuna taarifa za wagonjwa wapya kwa muda wa miezi miwili na kwamba tangu uanze, wagonjwa 2,185 wameugua na 20 kufariki dunia.

Maeneo yanayoongoza kwa uchafuzi wa mazingira na umwagaji holela majitaka yenye kinyesi ni Tandale, Manzese, Kigogo, Mabibo, Makuburi na kwa AlliMaua.

Mhowera amewataka wananchi kuzingatia kanuni za usafi na kutii sheria za afya na mazingira ili kuepukana na magonjwa ya milipuko.

error: Content is protected !!