Monday , 26 February 2024
Home Gazeti Makala & Uchambuzi Kingunge ametoweka akiwa ‘kijana’
Makala & UchambuziTangulizi

Kingunge ametoweka akiwa ‘kijana’

Spread the love

ALIYEKUWA “mchungaji mkuu” wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), msemaji wa chama hicho na muumini wa itikadi yake iliyokufa ya ujamaa, Kingunge Ngombale-Mwiru (87), amezikwa jana Jumatatu, jijini Dar es Salaam. Anaandika Saed Kubenea … (endelea).

Mwanasiasa mkongwe nchini, alifariki dunia katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, Ijumaa iliyopita. Amezikwa na maelfu ya watu wakiongozwa na Rais John Pombe Magufuli, kwenye makaburi ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.

Ngombale alifikishwa kwenye hospitali ya Muhimbili mwishoni mwa mwaka jana, baada ya kung’atwa na mbwa wake, tarehe 22 Desemba.

Ngombale, ni mmoja wa watu waliochangia juhudi za kupigania uhuru wa Tanzania na na baada ya uhuru akawa mtumishi mtiifu wa chama cha Tanganyika African National Union (TANU) na baadaye CCM.

Katika uchaguzi mkuu uliyopita, Ngombale alitangaza hadharani kuachana na chama chake hicho na kujiunga na kusema anajiunga na “mabadiliko.”

Kwa maneno yake mwenyewe, Ngombale alisema, “CCM hakina tena pumzi ya kuendelea kuongoza nchi. Nusu karne ya utawala wa kuanzia TANU hadi CCM unatosha kuonyesha jinsi madaraka yalivyowalewesha.”

Akitangaza uamuzi huo nyumbani kwake jijini Dar es Salaam, tarehe 4 Oktoba 2015, Ngombale alisema, “kuanzia sasa nawaachia chama chao.

Sikusudii kujiunga na chama chochote kwa sababu nimekuwa mwanaharakati kwa miaka 61 tangu kutafuta uhuru… nadhani hiyo miaka inatosha.

“Nusu karne ni muda mrefu sana. Kilichokuwa chama changu (CCM), hakiwezi kuleta jipya, kimeishiwa pumzi ya kuendelea kuongoza.

“Kuna msemo kwamba madaraka hulevya na madaraka ya muda mrefu hulevya moja kwa moja…kuongoza nchi ni kama kupanda mlima, unafika mahali pumzi zinakwisha, CCM imeishiwa pumzi ya kuongoza,” ameeleza.

Alisema nchi imefika mahala pagumu kiuchumi kiasi kwamba wananchi sasa wanataka mabadiliko ambayo yanaweza kuletwa na chama kingine na watu wapya na siyo tena CCM.

“Najua nguvu ya kupinga mabadiliko ni kubwa lakini kwa utafiti wa mzee kama mimi, najua nguvu ya kutaka mabadiliko ni kubwa zaidi kwa hiyo nawaambia wananchi wajiamini zaidi wakisubiri tarehe 25 ili wakapige kura,” alieleza mwanasiasa huyo mkongwe nchini.

Kingunge Ngombale-Mwiru alisema, nchi inakabiliwa na tatizo kubwa la uchumi na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, na kuwa njia pekee ya kuondoa umasikini ni kuhakikisha uchumi unakuwa kwa asilimia 10.

Alisema chini ya uongozi wa fikra mpya uchumi, unaweza kukua kwa asilimia 10 ndani ya miaka mitano kuanzia sasa na kwamba, inawezekana pia kufikia ukuaji wa asilimia 15 baada ya miaka 10.

Alisisitiza, “ndiyo maana nasema mabadiliko ni muhimu kweli kweli … tupate watu wengine wenye pumzi mpya. Nyinyi (CCM), pumzi imekwisha. Chama changu hiki kiwekwe benchi kidogo… na mimi nasema kikiwa chama cha upinzani, kiendelee kutoa mchango wake.”

Kwamba wakati Benjamin Mkapa alipoingia madarakani Novemba 1995, alikuta uchumi unakuwa kwa asilimia tatu hadi nne. Lakini alipokuwa akiondoka mwaka 2005, aliacha uchumi ukikua kwa asilimia saba.

“Mkapa aliacha sukari ikiuzwa kilo Sh. 600… hivi sasa sukari Sh. 2,000 na zaidi. Kwa miaka 10 ya uongozi wa Jakaya Kikwete, uchumi umekuwa kwa karibu asilimia saba. Maana yake ni kwamba kwa miaka 10, tumebaki palepale… yaani tumerudi nyuma.

“Mimi niko upande wa mabadiliko, tena yanahitajika sana. Nasema yamechelewa. Kama wasomi, wazee, wafanyakazi, wavuvi, wakulima na wafugaji wanataka mabadiliko lazima wana sababu.”

Alisema akiwa kama kada mkongwe wa Tanu hadi CCM kwa miaka 61, yeye na waanzilishi wengine walijenga chama chenye misingi imara ya kidemokrasia na kifikra wakiwa na mwelekeo wa mabadiliko kuanzia kudai uhuru, kuunganisha Tanganyika na Zanzibar hadi kukubali mfumo wa vyama vingi.

Lakini CCM anayoiona sasa ni ya watu wachache wenye malengo ya kufanya mambo wanayoyataka kwa maslahi asiyoyajua.

Kwa mujibu wa Ngombale, kwenye vikao vya CCM kikiwamo cha Halmashauri Kuu (NEC), hakuna mijadala ya maana kuweza kusaidia nchi na badala yake kinachofanyika ni kuajiri mavuvuzela na vijana kutukana wazee na makada wengine ndani ya chama hicho.

Alisema mtu anayeweza kuleta mabadiliko makubwa kiuchumi na kwenye nyanja nyingine ni mgombea urais wa Umoja wa Katiba ya Wananchi (UkAWA), Edward Lowassa.

Ngombale hakuwa kama wanasiasa wengine, wanaohubiri, lakini hawatendi. Yeye alikuwa akisema na kutenda. Katika uchaguzi huo wa mwaka 2005, Ngombale alipanda hadi kwenye majukwaa ya kisiasa kumnadi Lowassa.

Katika miaka ya mwisho ya uhai wake, Ngombale alikemea kwa nguvu kubwa uvujifu wa Katiba na kutaka mwananchi “kujisajili katika orodha ya wanaopinga uvunjifu wa Katiba na sheria za nchi.”

Alikuwa mtetezi mkuu wa haki ya vyama vya siasa ya kukutana na kuandamana. Alituhumu hadharani viongozi wenzake walionyamazia Katiba kusiginwa; na alimtaka Rais wa Jamhuri, Dk. John Magufuli, kuongoza nchi kwa busara.

Alieleza kuwa ili kunusuru nchi na hatari ya machafuko, ni vema Dk. Magufuli akutane na viongozi wakuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kujadili mustakabali wa taifa.

Alikuwa akirejea minyukano kati ya Chadema kilichotangaza 1 Septemba, kuwa siku ya maandamano na mikutano nchi mzima na serikali na CCM waliotangaza kupinga maandamano hayo.

Maandamano na mikutano ya Chadema imeitishwa kupinga kile inachokiita chama hicho, “nchi kupelekwe katika utawala wa kidikteta.”

Alisema, hatua ya rais kupuuza hoja ya kukutana na Chadema katika kipindi hiki cha kuelekea tarehe 1 Septemba, “yaweza kuingiza nchi katika madhara makubwa.”

Amesema, “namuomba Rais Magufuli, akubali kuitisha kikao na Chadema ambacho pia wazee wastaafu watahudhuria. Akifanya hivyo, …tutawageukia Chadema na kuwambia wasitishe mpango wao wa maandamano.”

Rais Magufuli ametengaza marufuku ya mikutano na maandamano ya kisiasa nchini kwa madai uchaguzi umekwisha; huu ni wakati wa kufanya kazi. Akaagiza wanaotaka kufanya siasa wasubiri mwaka 2020.

Akataka wanaotaka kufanya mikutano wakafanyie mikutano yao kule walikochaguliwa. Akadai yeye hajaribiwi na hajawahi kujaribiwa.

Ngombale ameonyesha kuwa amekuwa mtu wa mabadiliko. Ametetea haki ya Chadema na vyama vingine vya siasa nchini, kukutana na kuandamana.

Kitendo cha kuzuia kuandamana na kufanya mikutano, ni uvujifu wa katiba. Kinaweza kuingiza nchi katika machafuko.

Amewatuhumu hadharani baadhi ya viongozi wenzake, akiwamo marais wastaafu Benjamin Mkapa, Ali Hassan Mwinyi na Abeid Amani Karume, kwa kukaa kimya wakati Katiba inavurugwa.

Wengine aliowataja kunyamazia uvunjifu wa katiba, ni mawaziri wakuu wastaafu, Cleopa David Msuya, Joseph Sinde Warioba na Dk. Salim Ahemed Salim.

Akahoji, “…hawa wote wamewahi kula viapo vya utii kwa Katiba. Mbona wazee wenzangu mnakuwa kimya? Mnachokifanya siyo sahihi.”

Hakika, huyu ni Ngombale mpya. Siyo yule wa enzi za chama kushika hatamu. Anatambua kuwa hatamu zimeshakatika.

Amejiandikia historia yake nyingine, tena uzeeni. Amekemea serikali, ametetea katiba na ametaka kuwapo meza ya majadiliano kati ya upinzani na rais.

Ni jukumu la waliombwa kuzungumza, kulinda katiba, kuheshimu sheria na kuwa busara ya uongozi, kuamua kufuata ushauri wake wa kuutupa.

Lakini hataulizwa pale mambo yakiharibika. Hatalaumiwa. Hataombwa upatanishi kama ilivyokuwa huko nyuma. Hatapigiwa magoti.

Wala hataulizwa kwa nini alionya kuwa upande mmoja wenye raia ukililia katiba na sheria kufuatwa, serikali inaanda bunduki kuchinja raia.

Amesema, “laiti kama Chadema wangekuwa hawatetei Katiba na sheria, kungekuwa na kila sababu ya kuwashughulikia, lakini kwa kuwa wanatetea Katiba na sheria, kuna umuhimu wa kuyapa uzito madai yao.”

Amejiapiza na kuonya kuwa “hili ni suala la kila mtu anayependa utawala wa Katiba, Sheria na Utawala Bora.”

Kwa mujibu wa Katiba, ni haki ya kila raia kukutana na kuwa na uhuru wa mawazo; kufanya mawasiliano na kuchanganyika na kujiunga na vyama.

Aidha, Ngombale anajua kuwa taifa liko njia panda. Linapita katika barabara iliyosheheni mashimo, milima na mabonde.

Ndiyo msingi wa maneno yake, taifa linakabiliwa na ombwe la uongozi. Lina watawala, lakini limekosa watawala wenye maarifa ya kiuongozi.

Kwamba matamko kadhaa yaliyotolewa na baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini na taasisi za kiraia, yanathibitisha taifa kuwa katika mkwamo.

Kwamba matumaini ya wananchi kuwa maisha yatarejea kama kawaida baada ya kumalizika uchaguzi mkuu wa 25 Oktoba 2015, ghafla yameanza kutoweka.

Kwamba taifa lililokuwa likijinadi kuwa la amani na utulivu, linalosheshimu katiba na sheria, taratibu linaelekea kwenye kupalilia vitendo vya uvunjifu wa amani na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Kwamba vingi ya vitendo hivi, vinadaiwa kuratibiwa na mamlaka za serikali, kwa lengo la kuonea, kudhalilisha na kukandamiza haki za kiraia, ili kudumaza na kuviza demokrasia.

Ngombale alikuwa mmoja wa viongozi walioshiriki katika kutafuta mwafaka wa kisiasa Visiwani, tangu kuingia kwa mfumo wa vyama vingi nchini. Alianza mwafaka wa mwaka 1999, 2001 na hata wa mwaka 2008.

Mwafaka wa 1999 ulisimamiwa na Jumuiya ya kimataifa, huku mwafaka wa pili uliotokana na mauaji ya raia ya tarehe 26 na 27 Januari 2001, Unguja na Pemba, ulitekelekezwa na kusimamiwa na wahusika wenyewe.

Katika tukio hilo, watu 46 wanadaiwa waliuawa, wengine 658 wakajeruhiwa vibaya, watoto wakabaki yatima, wanawake wakaachwa wajane na wengine 135 wakapata ulemavu wa kudumu.

Ngombale alisema, ili serikali isirejee makosa hayo tarehe 1 Septemba, isijiruhusu kutenda ya Januari 2001. Kufanya hivyo, ni kuingiza nchi katika matatizo ya kisiasa, kiuchumi na kuibua mgogoro wa kidipromasia.

Ngombale alieleza mara kadhaa kuwa upinzani siyo uadui. Bali, ni serikali iliyoko njiani kuchukua madaraka, pindi yule aliyeko serikalini anaposhindwa kutekeleza matakwa ya wananchi.

Kuufanya upinzani ni uadui, ni kutaka nchi kuelekea kule ziliko baadhi ya nchi. Akasema, hatuhitaji kwenda huko. Lakini Ngombale amekufa bila kusikilizwa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Waliofariki ajalini Arusha kuagwa siku ya maandamano Chadema

Spread the loveMIILI ya watu 25 waliofariki dunia katika ajali iliyohusisha lori...

Habari za SiasaTangulizi

Serikali kuiburuzwa mahakamani ajali iliyoua 25 Arusha

Spread the loveMTANDAO wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), imeitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Samia atoa pole ajali iliyoua 25, kujeruhi 21 Arusha

Spread the loveRais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu...

Habari MchanganyikoTangulizi

25 wafariki dunia katika ajali Arusha

Spread the loveWatu 25 wamefariki dunia papo hapo mkoani Arusha katika ajali...

error: Content is protected !!