October 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kindamba apewa majukumu matatu Njombe

Waziri Kindamba, Mkuu wa Mkoa wa Njombe akiapa mbele ya Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amemkabidhi majukumu matatu, Mkuu mpya wa Mkoa wa Njombe, Waziri Kindamba. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Rais Samia ametoa maagizo hayo leo Jumanne, tarehe 15 Machi 2022, Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma, baada ya Kindamba kuapishwa kushika nafasi hiyo, iliyoachwa wazi na Mhandisi Marwa Mwita Rubirya, aliyestaafu.

Rais Samia, alimtaka Kindamba akapandishe mapato ya Mkoa wa Njombe, kwa kuwa ni miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri katika masuala ya uzalishaji mali.

“Anayeondoka amefanya kazi nzuri, naomba anzia hapo, ongeza jitihada nenda mbele. Njombe ni mkoa wenye kila kitu, kama utatulia unaweza ukapandisha kipato kwa kiasi kikubwa,” amesema Rais Samia.

Wakati huo huo, Rais Samia amemuagiza Kindamba akaondoe changamoto ya lishe kwenye mkoa huo, huku agizo lingine likiwa ni kuhamasisha utoaji wa chanjo ya Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19).

“Njombe ni mkoa unaozalisha chakula kwa wingi, tuna changamoto ya nutrition (lishe), hapo kaangalie vizuri, pia usisahau suala la chanjo, jitahidi shirikiana na wenzi kahamasishe watu wachanje, kama ulivyosikia tayari kuna omicron ameanzahuko Asia na akianza huko hawako mbali kuja kwetu, kwa hiyo kasimamie,” amesema Rais Samia.

Kindamba aliteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa Njombe, jana tarehe 14 Machi mwaka huu, akitoka kwenye nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), ambayo kwa sasa inashikiliwa na Peter Rudolph Ulanga.

error: Content is protected !!