September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kinana awaonya CCM, asema hakuna uchaguzi mwepesi

Abdulhaman Kinana

Spread the love

ABDULRAHMAN Kinana, Katibu Mkuu Mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), amewataka wanachama wa chama hicho, kushikamana katika kumtafutia kura za ushindi Rais John Magufuli, katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2020. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Leo Jumamosi tarehe 11 Julai 2020, Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM unaofanyika jijini Dodoma, wamemthibitisha kwa asilimia 100 Rais Magufuli kuwa mgombewa wa chama hicho katika nafasi ya Urais wa Tanzani.

Wajumbe wote 1822 wamempigia kura za ndiyo.

Awali, Kinana amewataka wajumbe wa mkutano huo, kumpa kura za ndio Rais Magufuli, ili awe mgombea, lakini pia wajitolee kwa hali na mali, kumtafutia kura kwenye Uchaguzi Mkuu.

Pia, Kinana amewataka WanaCCM kushikama katika kutafuta ushindi kwenye uchaguzi huo, katika nafasi za ubunge, wawakilishi na udiwani.

“Tunakwenda kwenye uchaguzi mkuu, nataka niwaombe WanaCCM tunafanye kazi kubwa ya mshikamano, kwa kujitolea kwa bidii kutafuta kura za mgombea ndugu John Magufuli, kutafuta kura za wabunge na udiwani,” amesema Kinana.

Aidha, Kinana amewataka wanachama wa CCM kutolaza damu kwa matumaini ya kwamba uchaguzi huo utakuwa rahisi kwa upande wao, kwa kuwa hakuna uchaguzi mwepesi.

“Hakuna uchaguzi ulio mwepesi, mmesikiliza jana mwenyekiti akisema tusidharau uchaguzi, uchaguzi ni pale kura zinahesabiwa na ushindi, lakini sina shaka hata kidogo mgombea wetu atapata kura kuliko alizopata mwaka 2015, pia tutapata wabunge na madiwani wengi zaidi” amesema Kinana.

Katika uchaguzi mkuu uliopita mwaka 2015, Rais Magufuli alipata kura milioni nane sawa na asilimia 58 huku mshindani kwake kupitia Chadema, Edward Lowassa akipata kura milioni sita sawa na asilimia 39.

Wakati huo huo, Kinana amewataka WanaCCM kujiepusha na makundi katika mchakato wa kutafuta wagombea wa ubunge, uwakilishi na udiwani.

“Hata tukiwa mia nawaomba tuzike tofauti zetu tuwe na mshikamano, tuweke mbele zaidi chama kuliko mtu, “ amesema Kinana.

Kinana ambaye alipewa adhabu ya kutoshiriki shughuli za CCM kwa muda wa miezi 18 na Kamati Kuu ya chama hicho kutokana na makosa ya ukiukwaji wa maadili na misingi ya CCM, ameshiriki Mkutano Mku wa CCM, baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho (NEC), kumsamehe.

Katibu Mkuu huyo mstaafu wa CCM, alipewa adhabu hiyo tarehe 28 Februari 2020 na Kamati Kuu ya CCM. Ambapo aliitumikia kwa takribani miezi minne, hadi aliposamehewa na NEC, kupitia kikao chake kilichoketi jana tarehe 10 Julai 2020, jijini Dodoma.

Msamaha huo umekuja baada ya mwanasiasa huyo miezi kadhaa iliyopita kuomba radhi hadharani, kufuatia makosa aliyoyafanya ya ukiukaji wa maadili ndani ya chama hicho.

error: Content is protected !!