Spread the love

 

MAKAMU wa CCM Bara, Abdulrahman Kinana ameonya viongozi wanaopata nafasi mbalimbali za kuteuliwa au kuchaguliwa kuacha tabia ya kutaka kutukuzwa kwani nafasi wanazopewa ni kwa jili ya kutumikia wananchi. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia amewasihi viongozi wa CCM kujifunza kutoka kwa mabalozi wa mashina ya chama hicho kwa namna wanavyotumikia chama kwa kujitolea.

Kinana ametoa kauli hiyo leo tarehe 10 Aprili, 2022 wakati akizungumza katika mkutano maalumu wa mapokezi yake ulioandaliwa na CCM mkoa wa Dar es Salaam.

Kinana ambaye wiki iliyopita alichaguliwa kwa kishindo kushika wadhifa huo wa Makamu wa CCM Bara, amewashukuru wajumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM kwa kumuamini nakumuunga mkono Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan aliyeteua kabla ya kupigiwa kura.

“Katika hivi vyeo tunavyopata kuna mila na desturi inaanza ya vyeo kuendana na utukufu na mbwembwe nyingi, niwaombe viongozi wenzangu kwamba kuchaguliwa kupewa uongozi ni utumishi wa umma, watakaokutukuza ni wale unaowatumikia utakapofanya kazi vizuri, ukijitukuza mwenyewe watakushusha,” amesema.

Aidha ametoa wito kwa wana CCM kujitokeza katika uchaguzi wa ndani wa chama hicho.

“Niwahimize vijana gombeeni, wakiwa na nafasi wapeni. Kina mama ni wengi kuliko kina baba kwa hiyo jitokezeni na wapeni nafasi,” amesema.

Aidha, amesema muda si mrefu Rais Samia ataitisha halmashauri kuu maalum ya CCM ambayo katika kikao hicho, atawaita mawaziri, lengo kutathimini hali ya uchumi wa nchi.

“Kikao kitalenga pia kuangalia namna tutakavyoharakisha maendeleo ya wananchi na kuangalia hali ya maisha kwa ujumla, kwa sababu Rais amesikia ugumu wa maisha

“Sina historia ya halmashauri kuu kukaa na mawaziri, kazi ya halmashauri kuu ni kutekeleza sera na kuisimamia, kuandaa ilani, kusimamia ilani. Kazi ya baraza la mawaziri ni kutekeleza ilani na kutekeleza ahadi za wananchi.

“Makundi haya yakikaa pamoja chini ya Rais Samia, tutatoka na majawabu mazuri ya kusaidia maendeleo ya Watanzania,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *