July 31, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kinachomtesa Magufuli ni woga

Spread the love

NCHI inatikisika. Kilicho nyuma ya mtikisiko huo ni woga wa mkuu wa nchi, Rais John Magufuli, tena woga usio na mchungaji, anaandika Faki Sosi.

Mambo mengi yanayoonekana kumpoteza Rais Magufuli kwenye nyoyo za Watanzania ni yale anayoweza kuyatibu.

Bila shaka, kama angekaa na wasaidizi wake na wasaidizi hao wakaondoa woga, Rais Magufuli angeendelea kutawala nyoyo za wananchi.

Rais Magufuli hapendi kukosolewa, anapotokea mtu na kumkosoa, huumia na kuhemuka, hili ndio tatizo kuu.

Katika hili, amepishana kwa asilimia kubwa na mtangulizi wake, Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete. Mkwere huyu (Kikwete) kwake maneno hayakuwa tija.

Na kama yalikuwa yakimuumiza basi aliwezi kuhimili mihemuko yake ingawa kwenye utawala wake waandishi waliathirika kwa kuvamiwa na wengine kuuawa.

Kwenye utawala wa Rais Kikwete, watu walikuwa huru kusema, kujadili na hata kugongana mawazo hadharani na kisha mjadala kuhitimishwa bila kutoana ngeu.

Hulka hii haipo kwa Rais Magufuli, anapoguswa hutaka kujitutumua kwa haraka na pale anapojitutumua mara nyingi hukosea. Hana subira.

Lakini pia wapinzani wanaposema jambo hata kama lina ukweli kiasi gani, yeye huliingia kwa pupa hatimaye hujikuta akizama ‘chaka.’

Kinachomtesa zaidi Rais Magufuli ni kutaka kupendwa, kuaminiwa na hata kushangiliwa na kila Mtanzania. Bila shaka atofanikiwa.

Jambo hili ndio linamtia doa kwa kuwa, anaamini kwamba ametawala nyoyo za Watanzania. Anaamini kuwa afanyalo ni lulu kwa Watanzania hivyo anayetokea kumkosoa, anakuwa adui yake.

Haamini kwamba, wapo walio na mawazo mbadala dhidi ya uamuzi wake, mawazo hayo kwake hataki kuyasikia. Anayempigia makofi na kumsifu, huyo ndiye rafiki yake, anayemkosoa anajenga uadui naye.

Naamini maisha kama haya ndiyo yanayomliwaza Rais Magufuli, lakini bila shaka hakuna taifa linaweza kuongozwa na kiongozi mwenye fikra za namna hii, asiyependa kukosolewa.

Rais Magufuli hatofurahia kuwa rais kama ataendelea kuwa na tabia hii. Taifa hili limeondoka kwenye mtazamo wa ‘zidumu fikra za mwenyekiti’ anapaswa kunong’onezwa hivyo.

Walio karibu naye wanapaswa kumweleza kuwa, dunia imehama na Tanzania imehama. Anapaswa kuishi kulingana na wakati na kwamba, sasa si zama za giza.

Anapaswa kuelezwa kuwa siku zinasonga mbele, waliomuona shujaa wanaanza kujutia, uamuzi wa kulipuka umewagusa na kuwaumiza.

Mashabiki wake wanaanza kupukutika. Waliomuona jasiri wanamuondoa kwenye fikra hizo, anaonesha kushindwa mapema.

Makundi yanayoonekana kutoridhika na utawala wake licha ya kumpamba wakati na baada ya uchaguzi yanadhihiri.

Wapo waliodhani Rais Magufuli ni shujaa katika utumbuaji majipu, lakini kumbe sivyo. Sakata la Kampuni ya Lugumu limemshusha, halizungumzi na wala hajihusishi. Watanzania wanajiuliza kulikoni? Kaishiwa nyembe ama sindano za kutumbulia?

Wapo wanaojadili ukanda kwamba, uteuzi wake unazingatia hivyo, hawa wanaoneshwa kutoridhishwa na hatua hii. Kundi hili tayari linamtazama tofauti.

Wapo wanaojadili ubaguzi. Ni kwa kuwa Baraza la Mawaziri aliloliunda limetelekeza Wazanzibari. Kwake Wazanzibari huenda si lolote si chochote.

Hii maana yake hata ile idadi ndogo ya Wazanzibari waliompa kura kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2015, watazidi kupungua. Hawa si wapumbavu, wanampa muda tu, hisabu yao ipo wazi.

Kundi lingine ni la Waislam, hawa wanaamini kwamba Rais Magufuli amewatelekeza. Wanaibua maswalia kwamba, wao hawajasoma? hawana nafasi kwenye utawala wake? ama hawakumpigia kura?

Wanajiuliza maswali hayo kutokana na uteuzi wake, ni kwa kuwa wanahesabu wanaotemwa na wanaosajiliwa kwenye serikali yake, ni katika ngazi zote.

Bila shaka kuongoza taifa lenye dini mbili na moja ikaonekana kulalamika kuelemewa, yapo madhara lakini tuombe yasitokee. Wapo waliomshangilia kwenye kundi hili na sasa wamemjengea chuki.

Kundi la waliopenda kuangalia matangazo ya moja kwa moja ya Bunge, nalo linamtazama kwa jicho la chuki. Kwa kuwa amezuia kupata huduma hiyo.

Mikutano ya hadhara amezuia, wapo wanaotaka kujua nini kianendela kutoka kwa viongozi wao na katika mkusanyiko ya hadhara. Hawa wamenyimwa uhuru huo, bila shaka amewachukiza.

Mteule wake ndani ya Bunge, Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika naye anakwenda kwa filimbi ya bosi wake (Rais Magufuli), yote haya yanaonekana wazi na kuchukiza wengi.

Idadi ya watu wengi waliokuwa wakimshabikia Rais Magufuli inapungua kila kukicha. Rais Magufuli anajitengenezea uadui mwenyewe hivyo anapaswa kujipima.

Katika yote hayo, anapotokea mtu na kukosoa, Rais Magufuli anaingia woga kwamba, wananchi wataelewa na wanaweza kumwona hafai. Hili ndio tatizo kuu.

Fikra hizi ndizo zinazomlazimu kuhakikisha anaminya sauti za wengi. Anachopaswa kuelezwa ni kuwa, woga huu ndio unammaliza na njia rahisi ni kuacha watu waseme na yeye asikilize.

Rais Magufuli anapaswa kujua kwamba, asitegemee kukosolewa na wabunge wa CCM, njia ya kujua wapi anapoteleza ni kuruhusu sauti huru kuvuma.

error: Content is protected !!