May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kina Mdee wamponza Nape bungeni

Nape Nnauye, Mbunge wa Mtama (CCM)

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai amemwonya Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye kuacha kuwasema vibaya, Halima Mdee na wenzake 18, kwamba hawastahili kuendelea kuwa wabunge. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

“Mdogo wangu Nape kuna maneno yalimtoka kidogo. Ana uhuru wa kusema, lakini kitu ambacho hana uhuru ni kuwasema vibaya wabunge wenzake, kwa kuwataja kwa majina,” amesema Spika Ndugai, leo Jumatatu, tarehe 3 Mei 2021, bungeni jijini Dodoma.

Spika Ndugai amesema alizungumza na Nape “na kwa kweli aliteleza, ninachowaomba ni kumsaheme bure.”

“Aliwakosea sana, aliwakosea sana, aliwakosea sana. Tuchunge sana midomo yetu hasa unapokuwa na mitizamo tofauti na ndiyo inayotusaidia kujenga nchi,” amesema

Tarehe 23 Aprili 2021, Nape akishiriki mjadala wa haki wa vyama vya siasa uliofanyika mtandaoni, alizungumzia sakata la Mdee na wenzake, baada ya kuulizwa maoni yake.

Nape alisema, kama Chadema iliwafukuza, basi Katiba inapaswa kulindwa kwa kuheshimu maamuzi ya taasisi ya kufukuzwa kwao.

Mdee na wenzake 18, walifukuzwa na kamati kuu ya Chadema tarehe 27 Novemba 2020 kwa tuhuma za usaliti, kughushi nyaraka za chama kisha kwenda bungeni, kuapishwa na Spika Ndugai kuwa wabunge.

Katika maelezo yake, Spika Ndugai amesema “Nape si tu alikosea, lakini Nape mdogo wangu, unaposhughulika na wanawake, ongea nao kwa heshima na hiyo iko hivyo dunia nzima.”

Soma Zaidi Hapa

Nape ashauri Mdee na wenzake wafukuzwe Bungeni

“Wanawake ni mama zetu, dada zetu na tunawapenda. Unaposhughulika na mtoto wa kiume ni tofauti na mwanamke, amesema

Mbali na Mdee aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), wengine ni, waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko, pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

Katika orodha hiyo, wamo pia Hawa Subira Mwaifunga, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa katibu mwenezi na Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar na Katibu Mkuu, Bawacha-Bara, Jesca Kishoa

Pia, aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.

Wengine waliofukuzwa Chadema, Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

error: Content is protected !!