August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kina Mdee waendelea kutinga, Dk. Tulia awaruhusu kuuliza maswali

Esther Matiko

Spread the love

 

WABUNGE wa viti maalum nchini Tanzania, Halima Mdee na wenzake 18 wasio na chama bungeni, leo Jumatatu tarehe 27 Juni 2022 wameendelea kuhudhuria vikao vya Bunge jijini Dodoma huku Spika wa Bunge hilo, Dk. Tulia Ackson akiwapa nafasi ya kuuliza maswali. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Wanahudhuria vikao vya Bunge ikiwa ni siku sita zimetimia tangu Mahakama Kuu, Kanda ya Dar es Salaam mbele ya Jaji John Mgeta kuyatupa maombi ya kuomba kufungua kesi kupinga kufukuzwa kwao.

Uamuzi huo ulitolewa tarehe 22 Juni 2022 kwa Jaji Mgeta kubainisha kasoro zilizobainika katika jina la mujibu maombi wa kwanza ambaye ni Chadema.

Jaji Mgetta alisema, Mdee na wenzake walipaswa kufungua maombi hayo kwa kutaja jina sahihi la bodi hiyo kwa mujibu wa sheria ambapo walitakiwa kuandika “Registered Body of Trustees” badala ya Body of Trusties, waliyoandika.

Kwa uamuzi huo Mdee na wenzake 18 walioapishwa tarehe 24 Novemba mwaka 2020 kuwa wabunge wa viti maalum walipoteza sifa za kuwa wabunge kwa mujibu wa Katiba ili uwe mbunge lazima uwe na chama cha siasa na wao kwa sasa hawana.

Tayari Chadema Ijumaa ya tarehe 23 Juni 2022 iliwasilisha bungeni barua kuhusu uamuzi huo wa Mahakama Kuu na nakala kuipeleka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.

MwanaHALISI Online limejitahidi kumtafuta Spika wa Bunge, Dk. Tulia ama Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi kujua kinachoendelea bila mafanikio.

Hata hivyo, leo Jumatatu tarehe 27 Juni 2022, ikiwa ni siku ya sita baadhi yao wamehudhuria kikao cha 52 kinachoongozwa na Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson.

Katika kikao hicho, baadhi ya waliopewa fursa ya kuuliza maswali ni, Esther Matiko, Tunza Malapo, Sophia Mwakagenda, Agnester Lambat, Ester Bulaya na Cecilia Pareso.

Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson

Mbali na Mdee, wengine waliofukuzwa Chadema, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati
Kuu (CC), Esther Matiko na Ester Bulaya; aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara), Hawa Subira Mwaifunga na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Wengine, ni aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza la Vijana la chama hicho (BAVICHA), Nusrat Hanje; aliyekuwa Naibu katibu mkuu wa Bawacha (Bara), Jesca David Kishoa; Cecilia Pareso, Agnesta Lambart, ambaye alikuwa mwenezi wa Bawacha na Tunza Malapa, aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema, mkoani Mtwara.

Katika orodha hiyo, wamo pia Asia Mohammed, aliyekuwa Naibu Katibu mkuu wa Bawacha (Zanzibar), Felister Njau, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Stella Flao, Anatropia Theonest, Salome Makamba na Conchesta Rwamlaza.

Mdee na wenzake walifungua maombi mahakamani kupinga kuvuliwa uanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), jambo ambalo lilikuwa linawafanya kupoteza sifa za kuendelea kuwa wabunge.

Walifikia uamuzi wa kukimbilia mahakamani, baada ya Kamati Kuu (CC) ya chama hicho, kuamua tarehe 27 Novemba 2020, kuwavua uanachama na baadaye mkutano wa Baraza Kuu wa 11 Mei 2022, kusikiliza rufaa zao na kufikia uamuzi wa kuwatimua.

Chadema walifikia uamuzi wa kumtimua Mdee na wenzake, ambaye alikuwa mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la chama hicho (BAWACHA), kufuatia kupatikana na makosa ya usaliti, kughushi nyaraka za chama na kisha kujipeleka bungeni kujiapisha kuwa wabunge, kinyume na maelekezo ya chama chenyewe.

error: Content is protected !!