Spread the love

 

LICHA ya Halima Mdee na wenzake 18 kufukuzwa uanachama ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), leo Jumatatu tarehe 16 Mei 2022 wameendelea kuhudhuria vikao vya Bunge jijini Dodoma. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Mdee na wenzake 18 walikata rufaa Baraza Kuu la Chadema kupinga kufukuzwa uanachama na kamati kuu ya chama hicho na rufaa hizo zilishindwa baada ya wajumbe 413 kati ya 423 kuunga mkono uamuzi wa kamati kuu.

Rufaa hizo zilisikilizwa katika kikao cha baraza kuu tarehe 11 Mei 2022 jijini Dar es Salaam na barua ya uamuzi huo kuwasilishwa ofisi ya Spika jijini Dodoma Ijumaa ya tarehe 13 Mei 2022.

Hata hivyo, baadhi yao walihudhuria vikoa Ijumaa na leo wameendelea kuhudhuria vikao hivyo na kupewa fursa na Spika Tulia Ackson kuuliza maswali ya nyongeza na msingi.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania miongoni mwa sababu zinazoweza kumfanya mtu akapoteza ubunge ni kufukuzwa uanachama wa chama chake.

Mdee na wenzake, walifukuzwa uanachama wa Chadema na Kamati Kuu ya chama hicho, 27 Novemba mwaka juzi na Jumatano iliyopita, Baraza Kuu likaridhia maamuzi hayo.

Katika mkutano wa Baraza Kuu, wajumbe 413sawa na asilimia 97 ya wajumbe 423 waliohudhuria – waliridhia Mdee na wenzake, kufukuzwa uanachama wa Chadema.

Walituhumiwa na kupatikana na hatia kwenye makosa kadhaa, ikiwamo kughushi nyaraka za chama, usaliti, uchonganishi, ugombanishi na kisha kujipeleka bungeni kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalum, kinyume na taratibu na maelekezo ya chama.

Mbali na Mdee ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa Chadema (Bawacha), wengine waliovuliwa uanachama, ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko; pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa baraza hilo, Grace Tendega.

Wengine waliofukuzwa Chadema, ni Hawa Mwaifunga, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa Katibu Mwenezi na Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Bawacha Zanzibar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *