December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kina Mbowe watumia kalenda kumhoji shahidi

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema na wenzake wakiwa mahakamani

Spread the love

 

MAWAKILI wa utetezi, katika kesi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, katika Mahakama Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, wamelazimika kutumia kalenda ya 2021, ili kumkumbusha shahidi wa jamhuri, Inspekta Lugawa Issa Maulid, siku husika ya tarehe 14 Novemba 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar ea Salaam … (endelea).

Tukio hilo limetokea leo Jumatano, tarehe 24 Novemba 2021, mahakamani hapo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, baada ya Inspekta Maulid, ambaye ni kaimu mkuu wa kituo cha Polisi cha Tazara, kushindwa kujibu swali la mawakili wa utetezi, kwa zaidi ya mara tatu.

Maswali hayo yalianza kuulizwa na Fredrick Kihwelo, aliyemuuliza Maulid kwamba tarehe 14 Novemba 2021 ilikiwa ni siku gani, ambapo alijibu akidai, hakumbuki hadi aangalie kalenda.

Aliulizwa swali hilo na Kihwelo, baada ya shahidi hiyo wakati akiongozwa kutoa ushahidi wake na Wakili Mwandamizi wa Serikali, Robert Kidando, kudai askari aliyemtaja kwa jina la Inspekta Swilla, kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI), alifika ofisini kwake, tarehe 14 Novemba 2021.

Akimtaarifu anahitajika kutoa ushahidi katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya, iliyotokana na mapingamizi ya utetezi, wakiomba yasipokelewe mahakamani hapo kwa madai kuwa hayakutolewa na shahidi huyo.

Kutokana na Inspekta Maulid kushindwa kujibu swali hilo, Wakili Peter Kibatala alimuomba Jaji Tiganga atumie kalenda aliyodai kuwa aliipata katika ofisi ya mahakama hiyo, kwa ajili ya kumkumbusha shahidi.

Baada ya kukubaliwa kuitumia, mahojiano yalikuwa kama yafuatavyo;

Kibatala: Isome (Kalenda) Inspekta Swilla alikuja ofisni kwako siku gapi?

Shahidi: Jumapili

Kibatala: Ulisema alifika Swilla Jumapili saa ngapi?

Shahidi: Saa tano asubuhi

Kibatala: Unasema ulifuatwa na mtu wa chumba cha mashtaka ofisini kwako ukashuka chini?

Shahidi: Ndio

Kibatala: Katika ushahidi wako kuna mahala popote uliiambia mahakama wewe ni kawaida yako kama kaimu mkuu wa kituo kufanya kazi siku ya Jumapili?

Shahidi: Nilimwambia kila siku lazima nifike kituoni

Kibatala: Siku ya Jumapili uliitaja?

Shahidi: Sikuitaja nilisema siku zote

Kaimu mkuu huyo wa Kituo cha Polisi Tazara Pugu Road, amemaliza kutoa ushahidi wake, ambapo alikileta kitabu cha kumbukumbu za mahabusu cha kituoni hapo, alichodai kuwa kinathibitisha kuwa Ling’wenya na mwenzake Adam Kasekwa, hawakuwekwa mahabusu katika kituo hicho kati ya tarehe 7,8 na 9 Agosti 2020.

Inspekta Maulid alitoa madai hayo, baada ya washtakiwa hao kuiambia mahakama hiyo kuwa walipokamatwa mkoani Kilimanjaro tarehe 5 Agosti 2020, walisafirishwa kuletwa Dar es Salaam, ambapo waliwekwa kwenye mahabusu ya kituo hicho.

Washtakiwa hao walitoa madai hayo wakati wakijitetea katika kesi ndogo ya kwanza ya kupinga maelezo ya onyo ya Kasekwa, yasipokelewe mahakamani hapo, wakida mtuhumiwa huyo hakuchukuliwa kama upande wa mashtaka ulivyodai kuwa aliyaandika katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, tarehe 7 Agosti mwaka jana.

Ling’wenya na Kasekwa walidai hawakuwahi kufikishwa katika kituo kikuu hapo, bali waliwekwa mahabusu Kituo chs Polisi Tazara na Mbweni.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi tarehe 25 Novemba 2021, itakapoendelea kwa shahidi wa tano kati ya sita watakaotoa ushahidi kwenye kesi hiyo.

error: Content is protected !!