January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kina Mbowe wapata kigugumizi kumkataa Jaji

Jaji Joachim Tiganga

Spread the love

 

CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema), kimedai Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na wenzake, wameshindwa kumuomba Jaji Joachim Tiganga,  ajiondoe katika kuisikiliza kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili, licha ya kwamba  hawana imani naye. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mbali na Mbowe, washtakiwa wengine katika kesi hiyo yenye mashtaka sita ya ugaidi,  ni waliokuwa Makomandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Halfan Bwire Hassan, Adam Kasekwa na Mohammed Abdillah Ling’wenya.

Kauli hiyo imetolewa leo Jumanne, tarehe 14 Desemba 2021 na Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika, baada ya Jaji Tiganga kuyatupa mapingamizi saba ya kina Mbowe na wenzake, katika kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Ling’wenya.

Mnyika aliamua kutoa kauli hiyo baada ya baadhi ya wafuasi wa Chadema, kuhoji kwa nini Kina Mbowe hawajamkataa Jaji Tiganga, kama walivyomkataa Jaji Elinaza Luvanda, baada ya kumtuhumu hawana imani naye.

Katibu Mkuu huyo wa Chadema amedai, Jaji Tiganga anastahili kukataliwa lakini wanashindwa kufanya hivyo, kwa kuwa itachukua muda  mrefu kupangiwa jaji mpya kutokana kwamba, Mahakama Kuu inaanza likizo kuanzia kesho tarehe 15 Desemba 2021, hadi Januari 31, 2022.

“Na kuhusu  jaji akataliwe nataka nilitolee kauli, hili jambo ni ukweli katika mazingira ya kawaida jaji huyu anastahili kukataliwa, lakini kwa ratiba ya mahakama kesho  tarehe 15 Desemba inaanza likizo  ambayo inakwenda mpaka tarehe 31 Januari. Jaji huyu angekataliwa leo mahakama ingepeta kisingizio, ingetumia likizo  kama misingi ya kusema Mbowe na wenzake wanaendelea kukaa gerezani, bila kuletwa mahakamani hadi tarehe 31, ” amedai Mnyika.

Mnyika amedai “tumeona mkakati wao hivyo  tusiwape mwanya kutumia kigezo hiki, tutaendelea naye pamoja na kwamba  hatumuamini, hatukubaliani naye na   amefanya maamuzi yasiuo ya haki ila tutaendelea.”

Wakati huo huo, Mnyika amedai kina Mbowe hawataweza kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo mdogo, hadi pale kesi ya msingi itakapomalizika na hukumu kutolewa.

“Hauwezi kukatiwa rufaa, ni uamuzi wa kati ambao hata kama haukubaliani nao hauwezi kuukatia rufaa sasa hivi.  Unatakiwa usubiri mpaka kesi ya msingi iishe ndipo mbele ya safari huko kwenye kesi ya juu ukihukumiwa unakatia rufaa. Tunafungwa mikono kisheria kwa sasa kuukatia rufaa, mbele ya safari tutaukatia rufaa ili usibaki kwenye mfumo wetu wa haki ukaja kuathiri wengine,” amedai Mnyika.

Aidha, Mnyika amedai  Chadema kinafanya uchambuzi dhidi ya maamuzi hayo, kisha kitatoa maoni yake.

Upande wa utetezi uliweka mapingamizi saba, ikiwemo lililodai mshtakiwa huyo hakuchukuliwa maelezo hayo katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, tarehe 7 Agosti 2020, bali siku hiyo alikuwepo katika Kituo cha Polisi Tazara , pingamizi lingine lilidai Ling’wenya alilazimishwa kusaini maelezo hayo katika Kituo cha Polisi Mbweni, katika Kituo cha Polisi Mbweni.

Mengine yalidai, maelezo hayo yalichukuliwa nje ya muda kisheria pamoja na  kuchukuliwa kwa sheria ambayo haipo .

Jaji Tiganga alisema, mahakama hiyo imeyatupa mapingamizi ya utetezi na kuyapokea maelezo hayo ya onyo kama kielelezo cha upande wa jamhuri, kwa kuwa yalirekodiwa kwa kufuata taratibu za kisheria.

Jaji Tiganga alisema, hoja za upande wa utetezi juu ya mapingamizi hayo hazikuwa na mashiko, kwani ushahidi wake haukuonesha mashaka katika ushahidi uliotolewa na jamhuri uliodai kwamba Ling’wenya alichukuliwa maelezo hayo kwa hiari yake, tarehe 7 Agosti 2020, katika Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam.

error: Content is protected !!