Monday , 29 May 2023
Home Gazeti Habari za Siasa Kina Mbowe wafunga ushahidi, uamuzi Desemba 14
Habari za SiasaTangulizi

Kina Mbowe wafunga ushahidi, uamuzi Desemba 14

Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema akiingia mahakamani
Spread the love

 

MAHAKAMA Kuu, Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, jijini Dar ea Salaam, imepanga kutoa uamuzi wa kesi ndogo ya kupinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa tatu, Mohammed Abdillah Ling’wenya yapokelewe au la tarehe 14 Desemba 2021. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Ni baada ya upande wa utetezi katika kesi hiyo ndogo ndani ya kesi ya msingi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake, watatu.

Tarehe hiyo imepangwa leo Jumatano, tarehe 1 Desemba 2021 na mahakama hiyo mbele ya Jaji Joachim Tiganga, baada ya upande wa utetezi kuomba kufunga ushahidi wake katika kesi hiyo ndogo.

Katika kesi hiyo, upande wa utetezi ulipinga maelezo hayo ya onyo yasipokelewe kwa madai si halali kwa mujibu wa sheria kwani hayakutolewa na mshtakiwa huyo.

Jaji Tiganga ameelekeza mawakili wa pande zote mbili kuwasilisha mawasilisho yao kwa njia za maandishi tarehe 7 Desemba 2021, ili kuandaa uamuzi dhidi ya kesi hiyo kama mahakama hiyo iyapokee maelezo ya onyo au isiyapokee.

“Maombi ya kuleta hoja kwa njia ya maandishi yanakubalika na mahakama inaamua tarehe 7 Desemba 2021 walete mawasilisho ya maandishi kurasa zisizozidi saba.”

“Mahakama itatoa uamuzi wake tarehe 14 Desemba 2021, washtakiwa  mtakua mahabusu mpaka tutakaposoma uamuzi,” amesema Jaji Tiganga.

Wakili wa Ling’wenya ambaye ni mshtakiwa wa tatu, Fredrick Kihwelo, aliomba wafunge ushahidi baada ya shahidi wao wa tatu, Gabriel Samheta Mhina, kumaliza kutoa ushahidi wake.

Mhina ambaye alikuwa ni Komandoo wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), alianza na kumaliza kutoa ushahidi wake leo, ambapo aliieleza mahakama hiyo namna alivyoingizwa kwenye kesi hiyo na kisha kuachwa huru kabla haijahamishiwa mahakani hapo ikitokea Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Alidai, aliachiwa huru tarehe 27 Juni 2021, baada ya Mbowe kukamatwa na kwamba upande wa mashtaka ulidai hauna nia ya kuendelea naye katika kesi ya uhujumu uchumi namba 63/2020 iliyokuwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Pia, Mhina alidai baada ya kukamatwa mkoani Tabora tarehe 19 Desemba 2020, alipatiwa mateso kwa kupigwa na kufungwa pingu muda wote. Pia alidai askari polisi waliomkamata hawakumuonya juu ya kosa lililokuwa linamkabili na wala hawakuandika taarifa zake katika kitabu cha kumbukumbu za mahabusu, katika vituo vya polisi alivyofikishwa.

Mbali na Mhina, mashahidi wengine wa utetezi walikuwa ni Ling’wenya mwenyewe aliyedai kwamba maelezo ya onyo yaliyoletwa mahakamani hapo na upande wa jamhuri hakuyatoa bali alilazimishwa kuandika nyaraka iliyodaiwa kuwa na maelezo hayo.

Ling’wenya alikanusha madai yaliyotolewa na aliyekuwa shahidi wa jamhuri, Askari Mpelelezi Msemwa, ya kwamba aliwekwa katika mahabusu ya Kituo Kikuu cha Polisi Dar es Salaam, tarehe 7 Agosti 2020 na kwamba yeye ndiye aliyemtoa kwa ajili ya kwenda kuchukuliwa maelezo.

Shahidi wa tatu wa utetezi alikuwa Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha), Mkoa wa Kilimanjaro, Lembrus Mchome, aliyedai Askari Msemwa hakuwepo katika kituo hicho 2020, akidai kuwa mwaka huo alikuwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay, Dar es Salaam, na kuwa alionana naye.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za SiasaTangulizi

Uamuzi juu ya wakurugenzi kusimamia uchaguzi 13 Juni

Spread the love  MAHAKAMA ya Afrika ya Haki za Binadamu (ACHPR), imepanga...

Habari MchanganyikoTangulizi

Jeshi la Polisi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika utafiti

Spread the love  JESHI la Polisi Nchini limesema kuwa katika kukabiliana na...

KimataifaTangulizi

Mtuhumiwa wa mauaji ya halaiki ya Rwanda akamatwa Afrika Kusini

Spread the love  MMOJA wa watuhumiwa wakuu wa mauaji ya Kimbari ya...

Habari za Siasa

Musoma Vijijini waomba ujenzi wa barabara uanze haraka

Spread the loveJIMBO la Musoma Vijijini, mkoani Mara, limeomba Serikali kuhakikisha ujenzi...

error: Content is protected !!