July 3, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kina Mbatia wafikisha kilio chao kwa Rais Samia, Dk. Mwinyi

James Mbatia, Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi

Spread the love

 

MGOGORO wa kiuongozi unaoendelea ndani ya Chama cha NCCR-Mageuzi umeendelea kukitikisa na upande wa Mwenyekiti, James Mbatia umeibuka na kuzitaka mamlaka zote zinazohusika kuchukua hatua za haraka kuumaliza. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Umetoa maombi hayo jana Jumanne tarehe 21 Juni 2022 nje ya ofisi ya msajili wa vyama vya siasa jijini Dar es Salaam walipoitikia wito wa msajili wa kuzikutanisha pande zote mbili zinazosigana ili kutafuta suluhu.

Msingi wa mgogoro huo unatokana na kikao cha halmashauri kuu kinachoelezwa kutokuwa halali kufanyika tatehe 21 Mei 2022 pamoja na mambo mengine waliazimia kumsimamisha uenyekiti Mbatia kutokana na tuhuma mbalimbali.

Baada ya mvutano wa hapa na pale wa upande wa Mbatia na ule wa Katibu Mkuu Martha Chiomba, tarehe 25 Mei 2022, ofisi ya msajili wa vyama vya siasa ilitoa taarifa kwa umma wa kumsimamisha Mbatia na sekretarieti yake yote kutojihusisha na siasa ndani ya chama hicho hadi uamuzi huo utakapoamuliwa vinginevyo.

Fukuto hilo likiendelea na kila upande kuushutumu mwingine, tarehe 8 Juni 2022, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Mohamed Ahmed alimwandikia barua Mbatia kumjulisha uwepo wa kikao cha pande hizo mbili ambacho kilikuwa kifanyike jana.

Hata hivyo, MwaanHALISI Online ambalo lilikuwepo eneo hilo kuanzia asubuhi, lilimshuhudia Mbatia akiongoza ujumbe wa upande wake akiwemo mjumbe wea bodi ya wakurugenzi, Sam Ruhuza, mwanasheria wa chama, Boniface Mwambukusi na Mkuu wa Idara ya Uenezi na Uhusiano wa Umma, Edward Simbeye.

Ilipofika saa 8 mchana, Mbatia na ujumbe wake ulitoka na Simbeye alizungumza na waandishi wa habari waliokuwapo nje ya ofisi hizo ambapo alisema walitii wito lakini Msajili wa Vyama, Jaji Francis Mutungi au Msajili Msaidizi, Sisty Nyahoza hawakuwapo n ahata upande wa mwingine hawakufika.

“Tumekaa na kujadiliana na machache ambayo Watanzania wanatamani kufahamu, tumekua wavumilivu kwa muda mrefu na jambo hili limekuwa ‘very serious’ kwani limetoka kwenye mambo ya kisiasa na limekwenda kwenye mambo ya udini, limekwenda kwenye U-tanganyika na U-Zanzibar,” alisema Simbeye

Alisema wameandika barua na malalamiko yao na kuyawasilisha ofisi ya msajili lakini ni wiki ya pili sasa hawajapata majibu ya msingi ya ambayo wanapaswa kuyapeleka kwa Watanzania.

“Watanzania na Serikali wanapaswa kufahamu, tumevumilia kwa muda mrefu, tumezuia vijana wasifanye jambo lolote kwa muda mrefu, sisi ni viongozi na sisi ni binadamu, tutashindwa kuwazuia vijana wetu na jambo hili litaleta shida kwenye nchi yetu,” alisema.

Joseph Selasini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya NCCR Mageuzi

Akizungumza kwa hisia, Simbeye alisema, “tunaitaka ofisi ya msajili kufanya uwajibikaji kwa haraka kwenye jambo hili na mamlaka zote zioneshe uongozi kwenye jambo hili, nchi inakwenda shimoni.”

“Jambo hili limetoka kwenye siasa limekwenda kwenye udini, U-tanganyika na U-zanzibar na tuna ‘fact’ zote na tumezipeleka kwenye mamlaka zote,” alisema

Simbeye alizitaka mamlaka ambazo wamezipelekea hoja hizo ni, Ofisi ya Rais, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Waziri Mkuu, Rais wa Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, “kuonesha fact za udini, ukabila na Utanganyika na Uzanzibar. Mamlaka zinazohusika zichukue hatua za dharura vinginevyo nchi inakwenda shimoni.”

error: Content is protected !!