Saturday , 20 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa CUF kwafukuta tena, Prof. Lipumba aonyesha maguvu yake
Habari za SiasaTangulizi

CUF kwafukuta tena, Prof. Lipumba aonyesha maguvu yake

Prof. Ibrahim Lipumba
Spread the love

MINYUKANO mipya ya kuwania madaraka, imeanza kujirudia kwa kasi, ndani ya Chama cha Wananchi (CUF). Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, hata kujiuzulu kwa aliyekuwa mkurugenzi wa habari na mawasiliano, Abdul Kambaya, swahiba mkuu wa Profesa Ibrahim Lipumba, kunatokana na vita hiyo ya madaraka.

Kwa mujibu wa afisa wa chama hicho, ambaye hakutaka kutaja jina lake akihofia kibarua chake, amesema kwa sasa chama hicho kinakabiliwa na migogoro, inayochangiwa na vita ya madaraka, hususan katika kipindi hiki ambacho Prof. Lipumba anapanga safu yake ya uongozi.

Anasema, ndani ya CUF, kuna makundi mawili yanayogombania vyeo, kundi la kwanza ni lile lililopambana kwenye mgogoro wa kiuongozi kati ya Prof. Lipumba, ambaye ni mwenyekiti wa chama hicho na Maalim Seif Sharrif Hamad, aliyekuwa katibu mkuu wake. Na la pili, ni la wale walioibuka baada ya mgogoro huo kuisha.

“Kuna vitu tunaweza kuongea ikaleta shida, unajua sisi tulivyo pale ni watendaji kama alivyokuwa afisa  mtendaji kata. Tunalipwa kwa mwezi,  tuko kazini. Yakikuta makubwa unaondolewa, ukiondolewa watoto wanakula nini?” amehoji afisa huyo na kuongeza:

“Maafisa tunakuwa wanyonge kutosema masuala ya chama. Sio kama sijui, najua lakini siwezi kukwambia mwanzo mpaka mwisho nahofia hayo, kuna vitu ukiongea tu, hata Prof. Lipumba atajua ni mtu fulani amesema.”

Akizungumzia sakata la kujiuzulu kwa Kambaya, afisa huyo amesema Kambaya hakushinikizwa ajiuzulu, isipokuwa, aliamua kukaa pembeni ili kukinusuru chama hicho, baada ya kuona majungu juu yake yanazidi.

“Mbona hela zinapita mbali sana kwake, kuna vijimajungu majungu, kile sasa nacho kimeleta jambo jipya sababu hata mimi sikutegemea, Kambaya hakuondoelwa kajiuzulu,” ameeleza.

Kufuatia hatua ya Kambaya Kujiuzulu, afisa huyo anaeleza kwamba, Prof. Lipumba ameamua kufanya mabadiliko ili kuzima sintofahamu iliyojitokeza kutokana na hatua hiyo.

“Mwenyekiti amefanya mabadiliko haya akiwa nje ya Dar es Salaam, kwa hiyo inaweka maswali mengi. Lakini ambacho naamini mpaka sasa, ni kama wamefunika jambo ili upepo upite,” ameeleza.

Akizungumzia migogoro inayoendelea chini kwa chini ndani ya CUF, amesema haitaisha kama viongozi wa chama hicho hawataamua kukaa chini kwa ajili ya kuisuluhisha.

“Ni kama kale kamgogoro ketu hakajaisha na kuelekea kwenye uchaguzi huko maana yake itazuka mengine. migogoro ndani ya chama haitapungua mpaka viongozi watakaposimamia vizuri kazi ya chama, yaani siasa ilivyo ni majungu na fitina ili yapungue ni kutafuta kazi ya kufanya,” amesema.

Amesema, “kukiwa na shughuli ya kufanya wataacha, sababu mkikaa muda mrefu bila kazi ni shida, kuondoka kwa mtu hilo halihusiani na operesheni za kazi, lakini hata lilivyo kaa liko tofauti na lilivyopokelewa.”

Afisa huyo amesema vita hiyo ilimuathiri hata yeye, ambapo aliwahi kusimamishwa kazi kwa zaidi ya miezi sita, bila ya kosa lolote.

Baada ya Kambaya kujiuzulu, Prof. Lipumba alimteua Mohamed Ngulangwa kuwa Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano na Umma.

Pia, alifanya mabadiliko kwa wakurugenzi, kwa kumteua Juma Kilaghai kuwa Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi akichukua nafasi ya Jafar Mneke, aliyeteuliwa kuwa Naibu Mkurugenzi wa Mambo ya Nje, Bunge na Sera.

MwanaHALISI ONLINE imetamfuta kwa njia ya simu Prof. Lipumba, aliyeko mkoani Tanga kwa ziara ya chama, kwa ajili ya ufafanuzi wa sakata hilo lakini simu yake haikupokelewa.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

BiasharaHabari za Siasa

Mavunde aagiza Perseus kuharakisha fidia Sengerema

Spread the loveWaziri wa Madini, Anthony Mavunde ameipongeza Kampuni ya Perseus kwa...

Habari za Siasa

Kigogo Chadema awanyooshea vidole vigogo serikalini kuhusu ripoti ya CAG

Spread the love  MWANACHAMA wa Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Boniface Jacob, amedai...

Habari za Siasa

Wabunge waikalia kooni TAKUKURU Bungeni

Spread the love  BAADHI ya wabunge wamelia na changamoto za utendaji wa...

Habari za SiasaTangulizi

Mpina ataka Waziri Majaliwa ajiuzulu, akosoa teuzi za mawaziri

Spread the love  MBUNGE wa Kisesa, Luhaga Mpina, amemtaka Waziri Mkuu, Kassim...

error: Content is protected !!