August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Kimbelembele’ cha Makonda chamtokea puani

Paul Makonda, Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam

Spread the love

SIKU moja baada ya Paul Makonda, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama mkoa, kutaka wahalifu wagongwe na kupigwa, huku akiikejeli watetezi wa Haki za Binadamu, sasa ameingia matatani,anaandika Faki Sosi.

Siku ya jana, Makonda alitoa kauli ya kulichochea Jeshi la Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, kufanya vitendo vilivyo kinyume na sheria pamoja na Haki za Binadamu.

Akiwa katika msiba wa askari watatu kati ya wane, waliouawa na majambazi huko Mbande katika tukio la ujambazi lililotokea 23 Agosti mwaka huu, Makonda alisema;

“Kamanda Sirro (Simon), mimi ndiye Mkuu wako wa Mkoa, nasema ukikutana na mtu yoyote kwenye msitu gonga, piga. Hao watu wa Haki za Binadamu wambie waje kwangu, hatuwezi kukaa kwenye mkoa ambao hauna usalama.”

Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imesema, “maagizo aliyotoa Mkuu huyo wa Mkoa hayana msingi wa kisheria na kwamba hayapo katika mamlaka yake.”

Taarifa iliyotolewa kwa wanahabari na Idara ya Elimu kwa Umma na Mafunzo ya tume hiyo, imenukuu kifungu cha 6(1)(f) na (i) pia kifungu cha 27 (1) na (2) (a) vya Sheria ya Tanzania, ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora sura ya 391 ya mwaka 2002.

Sheria hiyo na vifungu vyake inaipa mamlaka tume hiyo, kuchunguza mtu au taasisi yoyote kuhusiana na utendaji wa kazi zake, zinapokiuka mipaka ya madaraka yake.

Taarifa hiyo inaeleza zaidi kuwa, tayari Makonda ametumiwa barua ya wito, inayomtaka afike Makao Makuu ya tume hiyo tarehe 30 Agosti mwaka huu ili kujieleza, juu ya kile ambacho tume imekiona kuwa ni kejeli kwa tume hiyo na jumuiya zote za watetezi wa Haki za Binadamu.

error: Content is protected !!