August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kilosa walia na migogoro ya ardhi

William Lukuvi, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi

Spread the love

WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya makazi imeombwa kutatua changamoto ya migogoro ya mipaka iliyopo wilayani Kilosa mkoani Morogoro ili kuepusha hali ya maafa yanayoweza kutokea baina ya wakulima na wafugaji, anaandika Christina Haule.

Erasmo Tulo, mkurugenzi wa asasi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na utoaji wa elimu kwa jamii ijulikanayo kama Dira, amesema hayo jana wakati akitoa elimu ya masuala ya sera na sheria za ardhi katika vijiji 17 vya kata sita za wilaya ya Kilosa.

Tulo amesema anaiomba wizara hiyo kuchukua jitihada za dhati kutatua migogoro inayoonekana kuwachosha wananchi hao na kwamba kuchelewa kutatua kunaweza kukazua machafuko na kuleta uvunjifu wa amani ya eneo husika.

“Ni vyema wanawake wakaamka na kushiriki kikamilifu katika nafasi zote kimaendeleo ili kuhakikisha wanamiliki ardhi kisheria,” amesema.

Chiku Ally, mkazi wa Rudewa, Batini amesema wanawake wanashindwa kupata haki zao kufuatia suala la utatuzi wa migogoro hiyo kupitia mabaraza ya ardhi yaliyopo kugubikwa na rushwa.

“Wizara iingilie kati kwani tunashindwa kushiriki kesi katika mabaraza ya ardhi ya kata kwwani kuonesha ushahidi wa mipaka yao tunatakiwa kulipa kiasi cha Sh. 150,000/= hadi 200,000/= fedha ambazo ni nyingi kwetu kuweza kuzipata,” amesema.

Amesema migogoro hiyo inayohusisha mipaka kati ya vijiji na vijiji wilaya ya Kilosa imekuwa haitatuliwi kwa wakati kufuatia kugubikwa na masuala ya rushwa kwa maslahi ya viongozi waliopo kuanzia wenyeviti wa vijiji.

Naye Amina Zuberi ameiomba asasi ya Dira kuendelea kutoa elimu hiyo ili kuishawishi serikali kutatua changamoto hiyo ya mipaka kufuatia mgogoro wa kijiji chao cha Rudewa na Madoto kudumu ndani ya miaka 10 bila kupatiwa ufumbuzi huku wakikosa sehemu sahihi kwa ajili ya kilimo.

Alipohojiwa juu ya migogoro ya ardhi, Juma Mdangu mtendaji wa kijiji cha Rudewa, Batini amekana kuhusika kuzuia kukamilika kwa kesi za migogoro ya ardhi na kutotatuliwa kwa wakati na kudai katika kijiji hicho hakuna mgogoro wowote unaohusisha mipaka wala wananchi kugombea ardhi.

 

error: Content is protected !!