July 6, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kilio tozo mitandao ya simu: UVCCM wamuangukia Rais Samia

Baraka Shemahonge

Spread the love

 

UMOJA wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), mkoani Shinyanga, wameuomba Rais Samia Suluhu Hassan, apunguze kiwango cha tozo ya mitandao ya simu. Anaripoti Mwandishi Wetu, Shinyanga…(endelea).

Wito huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Shinyanga, Baraka Shemahonge, katika kikao cha baraza hilo, kilichofanyika mkoani humo na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Vijana, Kazi na Ajira, Patrobas Katambi.

Shemahonge alisema kuwa, tozo hiyo itapunguza ajira za vijana waliojiajiri katika biashara ya fedha za mtandaoni, kwa kuwa mzunguko wa miamala ya fedha itapungua, kutokana na watu kukwepa makato hayo.

‘Tunamuomba Rais Samia alitazame upya suala zima la tozo za miamala ya simu. Tunaona vijana wengi watakosa ajira, kwa sababu mzunguko wa miamala ya simu utapungua,” alisema Shemahonge.

Aidha, Shemahonge alisema, tozo hizo zitaathiri pia wananchi wa maeneo ya vijijini ambao wanategemea huduma ya fedha za mitandaoni kutokana na maeneo hayo kukosa huduma za benki.

Rais Samia Suluhu Hassan

“Lakini wazee na wananchi waliopo vijijini wataathirika, kwa sababu kule hakuna benki, wengi wanatumia simu katika kutuma na kupokea fedha, makato haya yanakwenda kuathiri moja kwa moja wananchi wenye kipato cha chini,” alisema Shemahonge.

Tozo hizo zilianza kutumika tarehe 15 Julai 2021, baada ya kupitishwa katika Bunge la Bajeti, lililoisha Juni mwaka huu.

Kwa mujibu wa tozo hiyo katika miamala ya simu, Serikali inatoza kuanzia Sh. 10 hadi 10,000 , katika muamala wa kutuma au kutoa pesa, kulingana na thamani ya muamala wa fedha husika.

Baada ya tozo hiyo kuanza kutumika, baadhi ya wananchi wameiomba Serikali ipunguze kiwango cha tozo hiyo.

error: Content is protected !!