November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kilio darasa la saba kunyimwa ajira serikalini chafikishwa bungeni

Mbunge wa Viti Maalum asiye na chama bungeni, Nusrat Hanje

Spread the love

MBUNGE Viti Maalum asiye na chama bungeni, Nusrat Hanje, amefikisha bungeni kilio cha wahitimu wa darasa la saba, wanaosoma katika Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), kukosa ajira serikalini. Anaripoti Nasra Bakari, DMC…(endelea).

Hanje amefikisha kilio hicho leo Alhamisi tarehe 27 Mei 2021, katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, bungeni jijini Dodoma.

Mbunge huyo viti maalum, amesema kumekuwa na changamoto ya wahitimu hao kupata ajira katika taasisi za umma, kwa kigezo cha kutokuwa na cheti cha kidato cha nne, licha ya kupata mafunzo katika vyuo vya VETA, vinavyotambuliwa na Serikali.

“Kumekuwa na ugumu wa kupata ajira kwa vijana hasa waliomaliza darasa la saba, kwenye taasisi za Serikali. Hata kama wamepata mafunzo katika vyuo vya ufundi vinavyotambuliwa serikalini , lakini wamekuwa wanapata ugumu wa kupata ajira kwa kigezo cha vyeti vya kidato cha nne ,” amesema Hanje na kuongeza:

“Serikali ina mkakati gani kuhakikisha inatambua vijana wetu ambao darasa la saba, wasiokuwa na vyeti vya kidato cha nne?”

Baada ya Hanje kuhoji hayo, Waziri Majaliwa amesema Serikali inaweka utaratibu wa kutatua changamoto hiyo.

“Katika mazingira ya kawaida ni kweli upo ugumu wa upatikanaji ajira, na changamoto ya ajira iko duniani kote ikiwemo Tanzania, lakini kila Serikali inaweka utaratibu mzuri kushughulikia changamoto hii,” amesema Waziri Majaliwa.

Waziri Majaliwa amesema Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan, inaendeleza mikakati iliyoachwa na Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya Hayati Rais John Magufuli, ya kutatua changamoto ya uhaba wa ajira, kwa kuhimiza ujenzi wa viwanda.

Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania

“Kwetu nchini Tanzania kupitia Serikali yetu inayoongozwa na Rais Samia, imeendeleza mkakati wa awamu ya tano wa kupanua wigo unaoruhusu Watanzania kupata ajira bila kuangalia elimu yao, bali muhimu ni ujuzi . Hasa waliopata mafunzo katika vyuo vyetu vya Serikali,” amesema Waziri Majaliwa na kuongeza:

“Mkakati wa ujenzi wa viwanda ndiyo jibu sahihi la kupunguza changamoto za ajira kwa ngazi zote, uwe umemaliza la saba au shahada, mkakati wetu wa ujenzi wa viwanda ni miongoni mwa njia muhimu kuwezesha upatikanaji ajira.”

error: Content is protected !!