MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kagaigai amesema mkoa huo umevunja rekodi kwa wananchi wake kuchangamkia chanjo ya Johnson&Johnson kudhibiti ugonjwa wa Covid-19 hali iliyosababisha dozi zote 60,000 zilizopelekwa mkoani humo kumalizika. Anaripoti Mwandishi Wetu, Kilimanjaro … (endelea).
Kagaigai ametoa kauli hiyo leo tarehe 15 Oktoba, 2021 wakati akizungumza katika mkutano wa ziara ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye yupo mkoani humo kwa ziara ya kikazi.
Kagaigai amesema baada ya wananchi wa Kilimanjaro kuchangamkia chanjo hiyo, waliomba kupewa dozi nyingine kutoka katika mikoa iliyosuasua na kupata dozi ya Johnson&Johnson 4,900.
“Tumeletwa dozi 4,900 na sasa zenyewe zipo katika harakati za kuisha… kwa hiyo tunashukuru kwa kujali maisha ya watu wa Kilimanjaro.
“Lakini sasa tumepokea dozi 36,864 za chanjo mpya aina ya Sinopharm ambazo ofisi za mkoa tunaandaa utaratibu wa kutoa elimu na kuisambaza kwa sababu chanjo hii inachanjwa mara mbili tofauti na ile ya Johnson&Johnson,” amesema.
Aidha, amesema mkoa wa Kilimanjaro umepokea fedha kiasi cha Sh bilioni nane ikiwamo ni sehemu ya mpango wa maendeleo kwa ustawi na mapambano ya UVIKO -19 ambao umetokana na mkopo nafuu wa Sh trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika hilo la IMF.
“Tutapokea magari ya kubebea wagonjwa zaidi ya saba, magari ya usimamizi na ufuatiliaji shughuli za afya na lishe kwa watoto na vifaa tiba vya aina mbalimbali,” amesema.
Rais Samia yupo mkoani Kilimanjaro ziara ya siku mbili hii ikiwa ni ziara yake ya kwanza ya kikazi mikoani tangu aliapishwa kushika madaraka Machi 19 mwaka huu.
Leave a comment