August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kilimanjaro, Mara, Morogoro vinara kipindupindu

Spread the love

MIKOA ya Mara, Kilimanjaro, Morogoro na Dar es Salaam ndio vinara kwa kuwa na wagonjwa wengi wa kipindupindi katika mwezi Aprili mwaka huu, anaandika Regina Mkonde.

Ummy Mwalimu, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ametoa kauli hiyo wizarani kwake leo wakati akieleza mwenendo wa ugonjwa wa kipindupindu.

“Mikoa inayoongoza kuwa na wagonjwa wapya wengi mwezi uliuoisha ni Mara 270, Kilimanjaro 198, Morogoro 188 na Dar es Salaam 90. Idadi ya vifo vilivyoripotiwa ni 16 wakati vifo vilivyoripotiwa mwezi Machi vilikuwa 47,” amesema Ummy.

Hata hivyo amesema, maambukizi ya ugonjwa kipindupindu nchini yamepungua kwa asilimia 65 ndani ya huo kutokana na kuwepo kwa idadi ndogo ya wagonjwa wanaopokelewa hospitalini.

“Takwimu za mwezi Aprili, 2016 zinaonesha kuwa kulikuwa na wagonjwa 1,037 idadi ambayo sawa na punguzo la asilimia 65 kutoka wagonjwa 2,953 walioripotiwa mwezi Machi mwaka huu,” amesema Ummy.

Amesema, katika mwezi ulioisha idadi ya wagonjwa ilikuwa ikipungua kila wiki kutoka 368 kwa wiki ya kwanza, 212 wiki ya pili, 143 wiki ya tatu hadi 104 wiki ya nne.

Aidha, Ummy ameitaja mikoa ambayo ugonjwa wa kipindupindu umedumu kwa muda mrefu kuwa ni Morogoro, Kilimanjaro, Mara, Pwani na Dar es Salaam.

“Mikoa ya Njombe na Ruvuma imefanikiwa kudhibiti ugonjwa wa kipindupindu kutokana na kutoripoti wagonjwa wa kipindupindu toka mlipuko uanze mwezi Agosti mwaka jana,” amesema.

Ummy amesema kuwa, takwimu zinaonesha kuwa hadi kufikia Mei 1, 2016 jumla ya wagonjwa 21,124 wameripotiwa na kati ya hao 331 wamepoteza maisha toka kuripotiwa kwa ugonjwa huo Mwezi Agosti mwaka jana.

Vile vile, ametoa onyo kwa wasimamizi wa huduma za Afya Mikoani na katika Halmashauri wanaoficha taarifa za wagonjwa wa kipindupindu.

“Yeyote atakayebainika kuwa anaficha taarifa hizi atachukuliwa hatua kali, wizara yangu inasisitiza kuwa juhudi za kusimamia kikamilifu hatua mbalimbaliza udhibiti wa mlipuko huu ziendelee,” amesema.

error: Content is protected !!