May 29, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kilichowaponza Askofu Gwajima na Jerry Silaa, kuhojiwa bungeni

Spread the love

 

SPIKA wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai ameagiza wabunge Askofu Josephat Gwajima na Jerry Silaa kufika mbele ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge ili kujibu tuhuma mbalimbali zinazowakabili ikiwemo kusema uongo na kushusha hadhi na heshima ya muhimili huo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dodoma … (endelea).

Wabunge hao wote wa chama tawala- Chama Cha Mapinduzi (CCM), endapo watakaidi kufika mbele ya kamati hiyo ambayo inaongozwa na mwenyekiti wake, Emmanuel Mwakasaka, watachukuliwa hatua za kisheria.

Taarifa ya kitengo cha mawasiliano na uhusiano wa kimataifa wa Bunge iliyotolewa leo Jumamosi, tarehe 21 Agosti 2021, imeeleza Gwajima ambaye ni mbunge wa Kawe atatakiwa kufika mbele ya kamati hiyo Jumatatu ya tarehe 23 Agosti 2021, saa 7:00 mchana katika ubunge 229 wa Bunge, Dodoma.

            Soma zaidi:-

Silaa yeye atafika mbele ya kamati hiyo kesho yake yaani Jumanne ya tarehe 24 Agosti 2021 saa 7:00 mchana katika ukumbi 229 wa Bunge.

Ingawa taarifa hiyo haikueleza tuhuma za wabunge hao, lakini katika siku za hivi karibuni, Gwajima ambaye ni Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, ameonyesha msimamo wake hadharani wa kupinga chanjo ya corona.

Askofu Gwajima amekuwa akitumia siku za Jumapili kuzungumza na waumini wa kanisa lake, lililopo Ubungo jijini Dar es Salaam kuwashauri wasichanje chanjo hiyo kwani ina madhara huku akisema yupo tayari kupoteza ubunge kama atalazimishwa kuchanjwa chanjo hiyo ili kuruhusiwa kuingia bungeni.

Kutokana na kauli hizo, Waziri wa Afya nchini Tanzania, Dk. Dorothy Gwajima amekwisha kuagiza Jeshi la Polisi na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kumkamata na kumhoji kutokana na tuhuma alizozitoa dhidi ya serikali akiwemo Rais wa Taifa hilo, Samia Suluhu Hassan.

Askofu Gwajima aliwatuhumu viongozi wa serikali kuhongwa fedha na watengenezaji wa chanjo hiyo ili kuiruhusu kuingia nchini. Rais Samia alizindua chanjo hiyo kwa kuchanjwa yeye mwenyewe tarehe 28 Julai 2021, Ikulu ya Dar es Salaam.

Kwa upande wake Jerry Silaa aliyewahi kuwa Meya wa Manispaa ya Ilala aliwahi kunukuliwa akizungumza na wananchi jimboni mwake Julai 2021 kuhusu suala la tozo za miamala ya simu akipendekeza na wabunge wawe wanakatwa kwenye mishahara yao.

“…mimi nimeanza ubunge Novemba mwaka jana. Ni wakati mwafaka kwa sisi wabunge ili tupate uwezo wa kusimama na kuwaeleza wananchi walipe kodi na sisi tulipe kodi kwenye mishahara yetu,” alisema Silaa

Hata hivyo, tarehe 3 Agosti 2021 ofisi ya Bunge ilitoa taarifa ya ufafanuzi ikieleza kwamba, wabunge kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na viongozi wa kisiasa nchini humo, wanakatwa kodi zote stahiki kwa mujibu wa sheria.

Miongoni mwa kodi hizo ni kodi ya mapato (PAYE), inayokatwa kwenye mishahara ya wabunge ya kila mwezi.

Taarifa ya Bunge ilieleza kinachoendelea mitandaoni kwamba wabunge hawalipi kodi kwenye mishahara hao hakina ukweli.

error: Content is protected !!