Thursday , 18 April 2024
Home Habari Mchanganyiko Kilichotokea kwa Maxence wa Jamii Forum kortini
Habari MchanganyikoTangulizi

Kilichotokea kwa Maxence wa Jamii Forum kortini

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam imeanza kusikiliza utetezi wa Wakurugenzi wa Jamii  Media Limited Maxence Mello na Mike William tarehe 5 Agosti 2019. Anaripoti Mwandishi Wetu …(endelea).

Melo ametoa ushahidi wake kwa kuieleza mahakama, kuwa polisi hawakujibu swali kwamba ni kifungu gani kinawaruhusu kupata taarifa za faragha za watumiaji wa mtandao wa Jamii forums?

Upande wa utetezi umeongozwa na wakili Peter Kibatala akishirikiana na Jebra Kambole, kwa upande wa mashtaka umewakiliswa na Sylvia Mitanto mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.

Mahojiano yalikuwa hivi:-

Kibatala: Mashitaka dhidi yako ni kwamba wanasema, ulizuia uchunguzi wa Jeshi la Polisi katika eneo la Mikocheni wewe na mwenzako mkiwa kama wakurugenzi wa Jamii Media inayoendesha JamiiForums; Polisi walitaka kuchunguza taarifa za Kampuni ya Oilcom (T) Ltd kuhusu tuhuma za member Fuhrer JF-Expert member, Je, ulikuwa Mkurugenzi wa Jamii Media LTD?

Maxence: Ni kweli kwa wakati huo nilikuwa mkurugenzi.

Kibatala: Wengine ni akina nani? wataje.

Maxence anawataja baadhi ya wakurugenzi.

Kibatala: Mike alikuwa mkurugenzi?

Maxence: Mike William hayumo, hakuwa mkurugenzi. Hata shahidi wa BRELA simkumbuki jina, alisema Mike sio mkurugenzi. Hakuna mtandao unaoendeshwa chini ya Jamii Media.

Jamii Media ilisajiliwa kuendesha na kufanya kazi ya matangazo sio mitandao ya kijamii. Ndiyo leseni yake ya biashara.

Kibatala: Kuna ushahidi wowote uliwahi kuletwa kuonesha kwamba Jamii Media imesajiliwa kuendesha mitandao ya kijamii?

Maxence: Hakuna ushahidi wowote ulioletwa.

Kibatala: JamiiForums ni nini?

Maxence: Ni mtandao wa kijamii ulianzishwa mwaka 2006 Machi mwanzoni ikiitwa Jambo Forums. Ni Social Network kwa ajili ya watu kutoa maoni mbalimbali na kushiriki mijadala anuai.

Kibatala: Kuna uhusiano gani wa kisheria kati ya Jamii Media na JamiiForums?

Maxence: Shahidi wa BRELA alisema ‘ule ni mwavuli’ tu. Hakuna uhusiano wowote wa kisheria. Shahidi yule alidai ni kwa kuwa aliona jina langu katika kampuni ya Jamii Media.

Kibatala: Watu wanatoaje maoni JamiiForums?

Maxence: Mtandao wa JamiiForums unatoa nafasi ya mtu yeyote kujisajili na kutoa maoni yoyote kwa jina lolote.

Kibatala: Kwenye hati ya mashtaka wanasema ninyi mnameneji, mnafahamu vipi Identity (utambulisho)0 ya mtu?

Maxence: Hatuna namna ya kufahamu identity ya member. Tunachoangalia ni maoni yake tu.

Kibatala: Hivi ni “Jamii Forum” au JamiiForums?

Maxence: Ni JamiiForums, ina “S”.

Kibatala: Mlikataa kutoa identity (utambulisho) yake, Fuhrer JF Expert Member, mngewezaje?

Maxence: Hatukuwa na uwezo huo.

Kibatala: Mahakama ingependa kufahamu Privacy (ufalagha) ni nini?

Maxence: JamiiForums inaelezea haki za mwanachama anapotumia mtandao huo. Sera yetu ya faragha ipo mtandaoni na kila mtu anaikuta kabla ya kujisajili anaisoma.

Kibatala: Ninapotaka kujiunga naiona?

Maxence: Mtu anapojiunga anaiona kwanza sera ya faragha.

Kibatala: Haya mambo ya falagha ni kwanini?

Maxence: Sheria za kimataifa zinazoongoza mitandao zinataka wamiliki wa mitandao kuwa Sera ya Falagha pia tuliangalia Katiba ya Tanzania, ibara ya 18 ambayo pia inalinda falagha ya mtu.

Kibatala: Mtu akijiunga JamiiForums, wewe unachokiona kinachomhusu ni nini?

Maxence: Tunaona jina alilojisajili na email (mpaka yeye aruhusu) kama hajataja email huwezi kujua.

Kibatala: Kuna ushahidi wowote uliletwa mahakamani kuhusu hii kesi ya Oilcom?

Maxence: Hakuna ushahidi wowote ulioletwa.

Kibalata: Kuna computer ililetwa mahakamani wakamuonesha hakimu kwamba taarifa za Oilcom zilizoandikwa JamiiForums ni hizi hapa?

Maxence: Hakuna

Kibatala: Kuna printout (nakala) yoyote iletwa mahakamani kumuonesha hakimu kwamba Fuhrer JF Expert Member, maneno yake aliyoyaandika ni haya hapa?

Maxence: Hakuna.

Kibatala: Wenzetu wa mashitaka wanasema walikuandikia barua, barua ya 23/2/2016 ilisainiwa na Fatma Kigondo. Ikiihusu Jamii Forum, Jamii Forum ni kitu gani?

Maxence: Sikijui.

Kibatala: Je, kwenye barua hiyo wanayosema walikuandikia, walitaja kifungu chochote cha sheria kinachowapa mamlaka ya kukuandikia barua? Walisema ni kifungu gani cha sheria?

Maxence: Hawakutaja.

Kibatala: Wanasema barua walimkabidhi Chrispine, ni lini Chrispine Muganyizi mwenye namba za simu 0714 xxxxx alikuja kutoa ushahidi mahakamani kuthibitisha kama kweli alipewa barua?

Maxence: Hajawahi kuja.

Kibatala: Ni lini mtandao wa Tigo walikuja kuthibitisha kwamba hizi namba walizotaja ni za Chrispine Muganyizi?

Maxence: Hakuna mtu aliyekuja.

Kibatala: Kuna ‘Dispatch’ (uthibitisho wa kupokea) iliyoletwa hapa mahakamani kuthibitisha kupokewa kwa hii barua ya polisi?

Maxence: Hapana

Kibatala: Kuna nyaraka barua ya 29/02/2016 ilisainiwa na Benedict Alex ambayo ipo hapa, ni (ID 1), Je unaitambua?

Maxence: Naitambua.

Kibatala: Huyo wakili unamfahamu?

Maxence: Ndio

Kibatala: Ana uhusiano wowote na Jamii Forums?

Maxence: Hapana. Aliandika kwa niaba ya Jamii Media Co. LTD na naomba mahakama iitambue kama ni majibu yetu kwa Jeshi la Polisi. (Kielelezo).

Kibatala: Hii barua ilikuwa inajibu nini?

Maxence: Tulikuwa tunarejea barua yao waliyotuandikia

Kibatala: Je, barua ilikuwa inaijibu P1?

Maxence: Ndio

Kibatala: Ilikuwa inajibu nini, soma hakimu asikie

Maxence: (Anasoma kilichojibiwa, anamsomea hakimu) kwamba tupo tayari kutoa ushirikiano iwapo watatueleza ni kifungu gani cha sheria wametumia kinachowapa mamlaka ya kutaka data za wateja wetu.

Kibatala: Je, mshawahi kujibiwa hiyo barua?

Maxence: Hatujawahi kujibiwa.

Kibatala: Mliahidi nini kwenye barua?

Maxence: Tuliahidi kutoa ushirikiano mkubwa endapo wangeeleza ni kwa mujibu wa sheria gani.

Kibatala: Polisi waliwahi kuja kuomba mahakama itoe amri ya kuwaamrisha ili nyie mtimize matakwa wanayoyataka?

Maxence: Haikuwahi kutokea kitu kama hicho.

Kibalata: Kuna maamuzi ya Mahakama Kuu ya Jaji Korosso na wenzake (Kitusi na Alfani), ambayo ni hukumu ya kesi ya Jamii Media dhidi ya Mwamasheria Mkuu wa Serikali (AG) na Mkuu wa Polisi (IGP) maamuzi yaliyotolewa Machi 8, 2017. Inakuhusuje?

Maxence:  Tulifungua shauri hili Mahakama Kuu baada ya kupata barua nyingi mfulizo kutoka polisi na TCRA tukiiomba mahakama isaidie kutafsiri barua hizo, kwani tuliona haki ya faragha inaenda kuvunjwa. Kesi hii tuliifungua kabla sijafunguliwa kesi hii (Machi 2016).

Kibalata: Angalia hii hukumu unaitambua?

Maxence: Naikumbuka. Ni hukumu ya Mahakama Kuu.

Kibatala: Mkabidhi wakili wa Jamhuri kama kielelezo.

(Wakili wa Serikali Sylvia Mitanto, anapinga kupokelewa kwa hukumu hiyo kama kielelezo).

Sylvia Mitanto: Sikubali hiki kielelezo kwasababu ni copy (nakala) sio original (halisi). Pia nahitaji nipate muda wa kutosha wa kuipitia hii hukumu.

Hakimu Simba: Tunatakiwa tupate majibu ya upande wa pili kuhusu hili pingamizi lilowekwa, hivyo Kibatala mnatakiwa mjibu tarehe 28.

Na nitatoa hukumu ndogo siku hiyo hiyo juu ya hili pingamizi kwamba hii hukumu ikubaliwe au la. Hii Kesi yetu haitakiwi kuvuka mwezi Septemba 2019 kabla ya hukumu.

Tarehe ya kujibu pingamizi la ushahidi ni 28 na 29 Agosti. Lazima tumalizane na kesi hii mwezi huu tusubiri hukumu.

Kesi imeahirishwa hadi tarehe 28 Agosti 2019.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

KimataifaTangulizi

Mkuu wa majeshi Kenya afariki, Ruto atangaza maombolezo

Spread the loveRais wa Kenya, William Ruto ametangaza maombezo ya siku tatu...

Habari Mchanganyiko

Carbon First, Ruangwa wasaini makubaliano ya biashara ya hewa ukaa

Spread the love  KAMPUNI ya Carbon First Tanzania Limited na Halmashauri ya...

Habari Mchanganyiko

CBE yawakumbuka wenye mahitaji maalum Jangwani

Spread the loveCHUO cha Elimu ya Biashara (CBE), kimetoa msaada mbalimbali na...

Habari za SiasaTangulizi

Chadema yatangaza ruti awamu ya pili maandamano

Spread the love  CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kimesema awamu ya...

error: Content is protected !!