Thursday , 25 April 2024
Home Gazeti Habari za Siasa Kilichomng’oa Lowassa Chadema hiki hapa
Habari za SiasaTangulizi

Kilichomng’oa Lowassa Chadema hiki hapa

Spread the love

WAZIRI mkuu aliyejiuzulu, Edward Ngoyai Lowassa, ametangaza kurejea katika Chama Cha Mapinduzi (CCM). Lowassa aliondoka CCM katikati ya mwaka 2015, kufuatia chama hicho “kumtosa katika kinyang’anyiro cha urais.” Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Taarifa zinasema, kurejea kwa mwanasiasa huyo kwenye chama tawala, kunatokana na shinikizo kutoka ndani ya familia yake na kile kinachoitwa, “kufungwa kwa njia yake ya kutaka kuwa mgombea tena wa urais kupitia Chadema.”

Ingawa upinzani haujataja mgombea wake, lakini anayepewa nafasi kubwa ya kugombea nafasi hiyo, ni Tundu Lissu, mbunge wa Singida Mashariki na Mnadhimu wa Kambi Rasmi ya Upinzani bungeni.

Kinachotajwa kuwa shinikizo la familia, taarifa zinasema, linatokana na kesi ya jinai inayomkabili mmoja wa watoto wake, Sioi Solomon.

Sioi mbaye aliyekuwa mwanasheria wa benki ya Stanbic, tawi la  Tanzania na wenzake wengine watatu, wanashitakiwa kwa makosa kadhaa, ikiwamo kula njama na kujipatia kwa udanganyifu, kughushi, utakatishaji wa fedha haramu.

Washitakiwa wengine, ni aliyepata kuwa Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA) na mwenyekiti wa kampuni ya Enterprise Growth Market Advisors Ltd (EGMA), Harry Kitilya; aliyekuwa mkuu wa idara ya ushirikiano na uwekezaji wa benki hiyo, Shose Mori Sinare na mwanasheria wa benki, Sioi Graham Solomon.

Washitakiwa wote wako gerezani tokea 1 Aprili 2016. Lowassa ameripotiwa akisema, alikutana na rais Magufuli na kumuomba kumsaidia kumtoa Sioi, ombi ambalo halikuwa limetekelezwa hadi anapotangaza kuondoka upinzani.

Lowassa ambaye alikuwa mpinzani mkuu wa Rais John Magufuli katika uchaguzi mkuu uliyopita, aliondoka CCM na kujiunga na Chadema, kupitia mkutano wake na waandishi wa habari wa tarehe 28 Julai 2015, katika hoteli ya Bahari Beach jijini Dar es Salaam.

Alichukua hatua hiyo, wiki moja baada ya jina lake kuenguliwa katika orodha ya wagombea urais wa CCM.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa  CCM haikumtendea haki katika kupitisha majina ya wagombea urais, hivyo hawezi kuendelea kubaki kwenye chama hicho.

“Niliwekewa mizengwe, kuhakikisha jina langu halifiki Kamati Kuu na Halmashauri Kuu (NEC). Nia yangu ni kuleta mabadiliko na kuondoka kwangu na kujiunga na Chadema, ni kuendeleza dhamira hiyo,” alieleza.

Aliongeza, “CCM siyo Baba yangu, wala siyo Mama yangu. Kama Watanzania wameyakosa mabadiliko CCM, basi watayatafuta kwingine. Ninaondoka. Sijakurupuka.”

Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, Lowassa aligombea urais kupitia muungano wa vyama vinne vilivyoko katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) na kutangazwa kushika nafasi ya pili nyuma ya Magufuli.

Hata hivyo, mwenyewe amekuwa akidai mara kadhaa kuwa kura zake ziliibwa.  Vyama vilivyomuunga mkono Lowassa katika kinyang’anyiro hicho, ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), NCCR- Mageuzi, Chama cha Wananchi (CUF) na National Legue Democrat (NLD).

Akizungumza katika ofisi za ndogo za CCM zilizopo Lumumba jijini Dar es Salaam, Lowassa alisema, ameamua kurejea nyumbani ambako sehemu kubwa ya maisha yake yamekuwa huko.

Lowassa alisindikizwa katika safari yake hiyo na aliyepata kuwa swahiba wake mkubwa, Rostam Aziz.

Rostam ambaye amepata kuwa mbunge wa Igunga (CCM) na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Uchumi na Fedha, ameibuka kuwa swahiba mkubwa pia wa Rais Magufuli.

Akiongea baada ya mapokezi hayo, Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli  amesema, wamempokea Lowassa na katika kuthibitisha hilo waliona ni vema uamuzi wake akautangazia Ofisi za CCM Lumumba.

Alisema, “tumetafakari na kujiridhisha kuwa Lowassa ameondoka kwa bahati mbaya. Tumemsikiliza mawazo yake na kwamba kutokana na sababu ambazo amezieleza, tumeamua kumpokea kwa mikono miwili. Amerudi nyumbani.”

Naye  Katibu Mkuu wa CCM Dk. Bashiru Ally amesema Lowassa amefikia uamuzi wa busara kwa kurudi nyumbani kwa ajili ya kushirikiana katika kuleta maendeleo ya wananchi wote

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Habari za Siasa

Kilosa yawa mfano wa kuigwa miradi ya Mwenge nchini

Spread the love  KIONGOZI wa Mbio za Mwenge Kitaifa Godfrey Mzava amezitaka...

Habari za SiasaTangulizi

Biteko ataja vipaumbele 7 bajeti nishati 2024/25

Spread the love  NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto...

Habari MchanganyikoHabari za Siasa

Mwekezaji amwaga bil. 39 kujenga viwanda 3 vya uchenjuaji

Spread the loveKampuni ya Mineral Access System Limited (MAST) inayoiwakilishwa kampuni ya...

Habari za SiasaTangulizi

Mpwa wa Magufuli mbaroni kwa kusambaza picha za utupu

Spread the loveJESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limewakamata...

error: Content is protected !!