December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kilichomkuta Maalim Seif CUF, chamnyemelea Prof. Lipumba

Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi

Spread the love

 

WALIOKUWA wajumbe wa Baraza Kuu la Chama cha Wananchi (CUF), wanatarajia kuwasilisha barua ya kukataa rufaa kupinga kutimuliwa, kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi, Jumanne ijayo. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Taarifa hiyo imetolewa leo Jumamosi, tarehe 13 Novemba 2021 na aliyewahi kuwa Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi, Uhusiano na Umma, Abdul Kambaya, akizungumza na MwanaHALISI Online, kwa simu.

Mbali na Kambaya, wengine waliofukuzwa ni, Ahmed Hamis, Mohamed Vuai, Ali Makame, Mtumwa Ambari, Dhifaa Mohamed Bakari na Chade Jidawi.

Kambaya ameueleza mtandao huu kuwa, yeye na wenzake waliofukuzwa CUF, wameshaandika barua na kwamba wanatarajia kuikifikisha kwa Jaji Mutungi, Jumanne ya tarehe 16 Novemba 2021, jijini Dodoma.

“Tumeshaandika barua na unajua hazipokelewi Dar es Salaam, zinapokelewa Dodoma, leo na kesho (Jumamosi na Jumapili), hawapo ofisini. Hivyo Jumatatu tutaenda Dodoma, kisha tutaikabidhi Jumanne,” amesema Kambaya.

Kambaya amesema kuwa, wanamuomba Jaji Mutungi atengue maamuzi ya baraza kuu la CUF, la kuwafukuza uanachama akidai halikufuata matakwa ya katiba ya chama hicho.

“Msingi wa barua yetu tulieleza kwenye mkutano kuna utaratibu wa katiba ulikiukwa, kuna wajumbe zaidi ya wanne wamepiga kura sio halali kwa mujibu wa katiba yetu ibara ya 81 (M), wale sio wajumbe wa baraza kuu,” amesema Kambaya.

Kambaya amesema “tunamtaka atengue maamuzi hayo, kwa mujibu wa katiba ya CUF.”

Mwanasiasa huyo amedai kuwa, katiba ya CUF inaelekeza wajumbe wa baraza hilo wanaotuhumiwa, kupiga kura wakati maamuzi hayo yanafanyika, lakini wao hawakupata nafasi hiyo.

“Sisi wenyewe hatukuruhusiwa kupiga kura, kinyume na ibara ya 81 (M), tulipaswa kupiga kura ya kufukuzwa au kuachwa,” amedai Kambaya.

Kambaya amedai kuwa, Kamati ya Nidhamu na Maadili iliyoandaa tuhuma dhidi yao, pia haikuwa halali.

“Kamati ya Nidhamu na Maadili iliyoleta tuhuma si halali, haikutimiza akidi hivyo tuhuma ni batili. Haikutimiza akidi na kuwa halali kusikiliza na kuamua hatima zetu,” amedai Kambaya.

Hivi karibuni akizungumza na wanahabari baada ya kufukuzwa, Kambaya alisema wameamua kufikisha mgogoro kwa msajili wa vyama vya siasa.

Kwani chombo chenye mamlaka ya kusikiliza rufaa yao ni Mkutano Mkuu wa CUF, ambao hufanyika mara moja kila baada ya miaka mitano.

Na kwamba hawana imani kama CUF itatenga fedha kiasi cha Sh. 600 milioni, kuitisha mkutano huo kwa ajili ya kusikiliza rufaa zao.

Kutokana na changamoto hiyo, Kambaya alisema wameamua kutumia ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kutafuta ufumbuzi wa mgogoro huo.

Kama walivyofanya katika mgogoro ulioibuka baina ya Mwenyekiti wa chama hicho, Prof. Ibrahim Lipumba na aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Hayati Maalim Seif Shariff Hamad.

Mgogoro wa Prof. Lipumba na Maalim Seif, aliyefariki dunia tarehe 17 Februari 2021, uliibuka baada ya mwenyekit huyo wa CUF, kufukuzwa na Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho, miaka mitano iliyopita.

error: Content is protected !!