April 17, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Kilichomkimbiza Meya wa Arusha Chadema, hiki hapa

Calist Lazaro, aliyekuwa Meya wa jiji la Arusha

Spread the love

MEYA wa jiji la Arusha, Calist Lazaro, ametangaza kuondoka ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema). Amewaambia waandishi wa habari, ameelekea Chama Cha Mapinduzi (CCM). Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea).

Lazaro alitangaza kuondoka chama hicho, jana Jumanne, ofisi ndogo za makao makuu ya CCM, Lumumba. Amepokelewa na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Hamphrey Polepole.

Lazaro amedai kuwa ameamua kuchukua uamuzi wa kuondoka Chadema, kufuatia kilichokuwa chama chake hicho, “kumzuia kufanya kazi na viongozi wa serikali.”

Taarifa za kuondoka kwa Lazaro ndani ya Chadema, zimekuja katika kipindi ambacho chama hicho kinajiandaa na uchaguzi wake mkuu wa ndani.

Lazaro anatajwa na wachambuzi wa masuala ya kisiasa kuwa alikuwa mmoja wa viongozi wa chama hicho, wenye ushawishi mkubwa katika eneo la Kanda ya Kaskazini. Kanda ya Kaskazini inaundwa na mikoa ya Arusha, Manyara, Tanga na Kilimanjaro.

MwanaHALISI ONLINE limeelezwa kuwa kabla ya kuwa meya wa jiji la Arusha, Lazaro alikuwa katibu wa Chadema mkoani Arusha. Alijiunga na chama hicho, akitokea Tanzania Lebour Party (TLP) ya Augustine Mrema.

Kwa mujibu wa taarifa zilizopo, Lazaro alikuwa na msuguano mkubwa na wa muda mrefu na mbunge wa Chadema katika jimbo la Arusha Mjini, Godblless Lema na hiyo, wapo wanaohusiha kuondoka kwake ndani ya Chadema na mgogoro huo.

“Hawa watu wawili (Lema na Lazaro), walifika mahali walikuwa hawaivi tena chungu kimoja. Kuna wakati Lema aliwasilisha hoja kwenye CC (Kamati Kuu), akitaka Lazaro ajadiliwe.

“Lakini CC ilimgomea. Ilisema maelezo ya Lema hayana ushahidi na yameletwa kienyeji na bila kuambatanisha ushahidi,” ameeleza mmoja wa wajumbe wa Kamati Kuu ambaye hakupenda kutajwa jina.

Amesema, “hivyo basi, kwa maoni yangu, kuondoka kwake, kunaweza kuwa kumechangiwa kwa kiwango kikubwa na fukuto lake na Lema. Na katika kuthibitisha hilo, ndio maana Lema amefurahia hatua ya Lazaro kuondoka Chadema.”

Akiandika katika ukurasa wake wa twitter, mara baada ya taarifa za Lazaro kujiondoa Chadema ma kujiunga na CCM kuvuja, Lema alisema, “kuondoka kwa Calist, kutaimarisha zaidi Chadema, kuliko kukidhoofisha.”

Alisema, “binafsi nimefurahi. Huyu bwana alikuwa CCM muda mrefu. Leo ndio ameamua kuvaa joho rasmi.Namtakia kila kheri.”

Akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kupokelewa ndani ya chama chake kipya, meya huyo wa zamani wa jiji la Arusha alisema, “leo Jumanne, tarehe 19 Novemba 2019, nimeamua kwa hiari yangu, kuondoka Chadema.”

Alisema, “nimechukua hatua hiyo, baada ya kujiridhisha kuwa ndani ya Chadema, watu wanachukiana bila sababu. Binafsi, nimesemwa na kusakamwa sana. Mara kadhaa, nimekuwa nikitundikiwa lundo la tuhuma, ikiwamo kuambiwa natumiwa na CCM.”

Lazaro anasema, mbali na matusi hayo, amepokea barua za maonyo kadhaa kutoka uongozi wa Chadema, zinazonitaka kutokutoa ushirikiano kwa viongozi wa serikali ninaofanya nao kazi kama meya.

Amesema, “nimekuwa nikifanya kazi katika mazingira magumu sana. nimeletewa barua nyingi za onyo kwa sababu ya kumsifia Rais Magufuli.”

Hatua ya Lazaro ya kujiunga na CCM, imemfanya kupoteza udiwani na umeya wa jiji la Arusha. Ndani ya Chadema, Lazaro amepoteza uenyekiti wa madiwani wa Chadema ambao ulimfanya kuwa mjumbe wa Kamati Kuu (CC) ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini.

error: Content is protected !!