August 16, 2022

Uhuru hauna Mipaka

‘Kila mkoa uanzishe Benki ya Wananchi’

Spread the love
KASSIM Majaliwa, Waziri Mkuu ameagiza kila mkoa nchini kuanzisha  Benki ya Wananchi, anaandika Dany Tibason.
Kauli hiyo ameitolea jana mjini Dodoma katika ufunguzi wa wadau wa Jumuiya za Benki ya Wananchi Tanzania (COBAT).
Waziri Majaliwa ametoa wito huo na kwamba, uanzishwaji wake unalenga kumkomboa Mwananchi katika suala la maendeleo.
Amesema, serikali ipo tayari kusaidia mikoa ambayo itachangamkia fursa hiyo kwa kuisaidia kwa hali na mali.
“Serikali itatazama juhudi za mkoa ndio itasaidia ila nitoe wito kwa kila mkoa  kuweka mipango mikakati ya kuanzisha Benki za Wananchi,” amesema Majaliwa.
Aidha amesema, serikali imeweka mikakati kwa kushirikiana na sekta binafsi ifikapo mwisho wa mwaka huu asilimia 50 ya watu wazima waweze kufikiwa kutumia huduma rasmi za kibenk kwa kupitia vikundi vya kuweka na huduma za mitandao ya simu.
“Hii ni kutokana na ukweli kwamba, huduma za kibenki na huduma zingine za kifedha ndio chanzo muhimu katika kuleta maendeleo na kupunguza umaskini, lengo ni kuhakikisha kwamba hatimaye wananchi wote nchini wanafikiwa na huduma hizi muhimu” amesema.
Majaliwa amesema, kwa sasa hapa nchini kuna vikundi 100,000 vya vikoba vyenye wanachama milioni 2.2 na mtaji wa shilingi Trioni 1.2.
Amesema, takwimu hizo zinaonesha kuwa asilimia 79 ya wanachama wa Vicoba ni wanawake na kwamba, changamoto iliyopo katika sekta hiyo ni wananchi wengi wanaoishi vijijini kutopata huduma rasmi za kifedha.
Amesema, hadi mwishoni mwa mwaka 2015 Benki za Wananchi zilizo na wanachama Cobat zilikuwa na jumla ya mali iliyofikia Sh. 86.3 bilioni ambapo amana za wateja zilifikia Sh. 69.2 bilioni na mikopo kwa wateja ilifikia Sh. 56.2 bilioni.
Dk.Philip Mpango, Waziri wa Fedha na Mipango amesema, Benki za Wananchi zilianza mwaka 1995 ambapo Benki Kuu ya Tanzania ilitoa leseni kwa Benki ya Wananchi wa Kilimanjaro.
Amesema, benki hizo zinasimamiwa na Benki Kuu ya Tanzania chini ya sheria za benki na taasisi za fedha ya mwaka 2006.
“Kwa hiyo ni muhimu kwa wadau kuhamasisha uanzishaji na uendelezaji wa benki hizo katika mikoa, hii inawezekana iwapo wananchi, benk za jamii na halmashauri wasatahamasishwa kununua hisa katika Benki za Wananchi,’’ amesema.
Elizabeth Makwabe, Mwenyekiti wa Cobat amesema, Benki za Wananchi ni kama dhahabu iliyojificha chini ya ardhi hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, wanaowajibu wa kuandaa mikakati ili kuleta ufanisi.
“Ili kufanikisha uanzishwaji wa benki za Wananchi katika kila Mkoa na baadae kila Wilaya serikali ni lazima iwe mhamasishaji hasa kupitia halmashauri za wilaya,’’ amesema.
error: Content is protected !!